Na Shamimu Nyaki - WUSM
Mkurugenzi Msaidizi Lugha, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Resan Mnata ametoa wito kwa Wadau wa Utamaduni kujitokeza kufadhili na kuunga mkono shughuli za Utamaduni nchini.
Dkt. Mnata ametoa rai hiyo Julai 23, 2022 Chamwino Dodoma, wakati wa Tamasha la 13 la Muziki wa Cigogo katika Kijiji Cha Chamwino Ikulu.
Aidha, Dkt. Mnata ametoa pongezi kwa Dkt. Kedmon Mapana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambaye ndiye mwanzilishi wa Tamasha hilo ambalo limesaidia kueneza na kukuza Mila na Desturi za Wagogo.
Pia Dkt. Mnata ameitaka mikoa mingine kufanya matamasha kama hayo katika kukuza na kuendeleza mila,t amaduni na desturi ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Vilevile, Dkt. Mnata ametoa wito kwa jamii kujitokeza kwa wingi Agosti 23, 2022 kuhesabiwa.
Tamasha la Cigogo linalofanyika kwa siku tatu Julai 22 hadi 24, 2022 likiongozwa na Kauli Mbiu "Elimu ya Sanaa ni Muhimu kwa Maendeleo Endelevu " linapambwa na ngoma mbalimbali za kitamaduni kutoka kabila la Wagogo Dodoma.
Watumishi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wenyeji wa Dodoma na wageni kutoka nje wameshiriki katika Tamasha hilo.