Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Kijaji: Fedha za Maboresho Shule Kongwe Zitumike kwa Lengo Lililokusudiwa
Feb 13, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_40411" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe Bi. Annisia Mauka, akisoma taarifa ya utekerezaji wa maboresho ya Shule hiyo yaliyogharimu takribani Sh. bilioni 1.374, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), Wilayani Korogwe MkoaniI Tanga.[/caption]

Na Peter Haule, WFM, Korogwe

Serikali imewataka watendaji katika maeneo yote ambayo fedha zimetolewa zikiwemo sh. bilioni 18 za kuboresha shule kongwe nchini, kusimamia matumizi yake ipasavyo ili kufikia lengo lililokusudiwa na kwa ubora unaotakiwa.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, alipotembelea na kukagua maboresho ya Shule Kongwe ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Mkoani Tanga, ambayo hivi sasa imekuwa ya kisasa na mwonekano mzuri.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imeamua kutekeleza kazi zake nyingi kwa mfumo ujulikanao kama Force Account, ambao unatoa fursa kwa Wakandarasi wazawa kushiriki kikamilifu kwa lengo la kufanikisha maendeleo kwa gharama nafuu na kwa ubora unaotakiwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, Bi. Annisia Mauka, katika taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya shule hiyo, alisema,   Serikali, kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) iliwapatia kiasi cha  Sh. bilioni1.3 kwa ajili ya kujenga miundombinu 27 ya Shule, ikiwemo umeme, majisafi na taka na pia Mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

[caption id="attachment_40413" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na Marietha Yohana na wanafunzi wengine wa kidato cha kwanza ambao ni walemavu, katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe ambapo alisema wana nafasi ya kufanya vizuri katika masomo yao na kuwa msaada mkubwa kwa Taifa siku za usoni.[/caption]

“Tumefanikiwa kukarabati majengo 26 ambayo ni pamoja na  vyumba vya madarasa 23,  maabara, maktaba, jengo la utawala, mabweni, bwalo la chakula, vyoo vyenye matundu 116, jengo la Zahanati, Mfumo wa Maji taka na safi na pia mfumo wa kupikia kwa njia ya nishati ya gesi” alifafanua Bi. Mauka.

Alisema kuwa hadi sasa fedha zilizotumika kununulia vifaa ni takribani Sh. bilioni 1.05 huku gharama za ufundi zikiwa Sh. milioni 315.9 hivyo kusalia na zaidi ya Sh. milioni 2.09.

Bi. Mauka, ameiomba Serikali kufanikisha ujenzi wa Bweni jipya linalogharimu zaidi ya Sh. milioni 109.6 kwa kuwa Bweni hilo lilishindikana kufanyiwa maboresho kwa kuwa uharibifu wake ulikua mkubwa baada ya kufanyiwa tathmini ya kina, pia aliiomba Serikali kufanikisha ujenzi wa ukuta wa Shule hiyo kwa kuwa kukosekana kwa ukuta huo kunahatarisha usalama wa wanafunzi na watumishi wengine.

[caption id="attachment_40414" align="aligncenter" width="750"] Wanafunzi wa kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe wakifanya Jaribio la Somo la Uraia, wakati wa ziara ya Kikazi ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Shuleni hapo.[/caption]

Naibu Waziri Dkt. Kijaji, ameahidi kufanyia kazi maombi hayo kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mhe. Mary Chatanda, na kutoa agizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, kufanya tathmini ya gharama ya ukuta huo ili kujua gharama halisi  kwa lengo la kupata fedha za ujenzi ili kulinda usalama wa Wanafunzi.

Dkt. Kijaji, aliupongeza Uongozi wa Shule na Wadau wengine kwa kuwezesha ukarabati Mkubwa wa Shule hiyo hivyo kurudisha hadhi yake na kuwa sehemu bora ya wanafunzi kupata taaluma kwa viwango vya juu.

Akizungumza na wanafunzi wa Shule hiyo Dkt. Kijaji aliwataka kusoma kwa bidii ili kuweza kufaulu masomo yao na kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa na pia kuwa viongozi imara wa baadae.

Jumla ya Sh. bilioni 18 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ukarabati wa Shule Kongwe za Sekondari 17 kuanzia mwaka wa Fedha 2016-2017.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi