Hamza Temba, Mlele Katavi
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani Katavi kumkamata na kumfungulia mashtaka Mkuu wa Kanda - Pori la Akiba Rukwa, Emannuel Barabara kufuatia tuhuma za uhujumu uchumi zinazomkabili.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miezi mitatu tangu alipomsimamisha kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo ambazo amesema tayari zimethibitishwa kupitia taarifa mbalimbali za kiuchunguzi.
Waziri Kigwangalla ametoa agizo hilo jana muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya Wilaya ya Mlele iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Wilaya hiyo, Rachel Kasanda wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo.
Amesema Barabara anatuhumiwa kwa vitendo vya uhujumu uchumi kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo pamoja na kushirikiana na majangili kuruhusu uvunaji holela wa raslilimali za misitu ndani ya pori hilo kwa maslahi yao binafsi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda alisema katika kipindi cha mwezi Desemba 2017 hadi Februari 2018 kamati yake ya ulinzi na usalama ilipata taarifa za uvamizi mkubwa katika Pori la Akiba Rukwa ambapo iliamua kufanya operesheni maalum iliyosaidia kukamata watu 22 waliokuwa wakichana mbao na kukamata mbao 5,122, slipa 924 na magogo 188.
Alisema kwa kiasi kikubwa uhalifu huo ulichangiwa na ndugu Barabara ambaye hakutaka kuweka wazi uhalifu uliokuwa ukifanyika ndani ya pori hilo kwa kamati yake ya ulinzi na usalama na badala yake aliiaminisha kuwa mambo ni shwari ndani ya pori hilo.
Halikadhalika, Dk. Kigwangalla ameagiza maofisa na askari wote 34 wa Pori la Akiba Rukwa kurudishwa makao makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ili kupangiwa kazi nyingine, ambapo kabla ya zoezi hilo ameagiza wahojiwe na TAKUKURU kuhusu mwenendo wa vitendo vya Mkuu wa Kanda hiyo, Emmanuel barabara na endapo nao watathibitika kuhusika wafunguliwe mashtaka ya kushirikiana nae katika tuhuma zinazomkabili.
Wakati huohuo Waziri Kigwangalla amemsimamisha kazi, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu wa wilaya ya Mlele, Ezeckiel Mbilinyi na watumishi wengine watatu kwa kile alichokieleza kuwa ni uzembe wa kushindwa kusimamia vizuri rasilimali za misitu wilayani humo sambamba na tuhuma za kushirikiana na ndugu Emmanuel Barabara kuhujumu rasilimali za misitu kwa kutoa vibali na kugonga nyundo (mihuri) rasilimali hizo zilizokuwa zikivunwa kinyume cha sheria kwenye maeneo ya hifadhi.
Kufuatia uamuzi huo, Dk. Kigwangalla ametangaza kusimamisha zoezi la utoaji wa vibali vipya vya uvunaji na usafirishaji wa mbao na magogo kwa mikoa ya kanda ya magharibi ikiwemo Katavi na Tabora kwa kipindi cha miezi mitatu mpaka hapo utaratibu mzuri utakapowekwa wa kudhibiti uvunaji wa rasilimali hiyo kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria.
Aidha ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Mlele kufanya uhakiki wa vibali vya uvunaji wa mbao na magogo ambavyo vimeshatolewa ili kujiridhisha juu ya uhalali wake kabla ya kutoa vibali vya usafirishaji.