[caption id="attachment_48684" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwasilisha Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Alifanya uwasilishaji huo Novemba 6, 2019 Dodoma.[/caption]
Na: Veronica Simba - Dodoma
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amewasilisha Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Waziri aliwasilisha Mkataba huo Novemba 6, 2019 kwa Kamati husika iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mariam Ditopile, ikiwa ni hatua kuelekea uwasilishwaji wake kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 14 mwaka huu, ili kuomba uridhiwe.
[caption id="attachment_48685" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwasilisha Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Alifanya uwasilishaji huo Novemba 6, 2019 Dodoma. Wa pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.[/caption]Waziri aliiambia Kamati kuwa ili Tanzania inufaike ipasavyo na Mkataba wa ISA, ipo haja ya kuuridhia kwa lengo la kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa nishati bora itokanayo na jua, kukuza teknolojia ya matumizi ya nishati jua na kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na uchafuzi wa hewa ukaa nchini.
Akitaja faida mahsusi ambazo Tanzania itapata kutokana na Mkataba huo, Waziri alisema kuwa ni kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme nchini hususan katika maeneo ya vijijini ambayo itachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kukuza vipato vya wananchi.
Pia, alisema faida nyingine ni kuongezeka kwa matumizi ya nishati safi na bora nchini na hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na uwepo wa hewa ukaa.
[caption id="attachment_48687" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya viongozi na wataalam wa Wizara ya Nishati, wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa akiwasilisha Mkataba wa Kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Alifanya uwasilishaji huo Novemba 6, 2019 Dodoma.[/caption]Nyingine ni kukua kwa teknolojia ya umeme jua nchini, kuongezeka kwa utaalamu na ujuzi kwa watanzania kunakotokana na fursa za mafunzo pamoja na kuimarika kwa uwekezaji katika miradi ya nishati ya jua hususan kutoka sekta binafsi.
Alisema, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 inatambua umuhimu wa kuendeleza vyanzo mbalimbali vya nishati mbadala na jadidifu ikiwemo nishati ya jua.
Akifafanua zaidi, Waziri alieleza kuwa kupitia ushirikiano wa ISA, takribani nchi 121 zilizopo katika Ukanda wa Tropiki ya Kansa na Kaprikoni ambazo zinapata nishati ya jua kwa wingi zinahamasishwa kufanya jitihada za pamoja katika kutumia nguvu ya jua kuzalisha umeme.
Hadi kufikia mwezi Oktoba, 2019 jumla ya nchi 79 kati ya 121 zilikuwa zimeshasaini Mkataba wa ISA ikiwemo Tanzania ambayo ilisaini mwezi Novemba, 2016. Nchi 57 kati ya zile zilizosaini tayari zimeridhia Mkataba huo.
Viongozi mbalimbali wa Wizara akiwemo Katibu Mkuu, Dkt Hamisi Mwinyimvua, walishiriki katika tukio hilo.