Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Mohamed Gaber Abulwafa katika Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam leo Agosti 18, 2022.
Pamoja na mambo mbalimbali, kikao hicho kimezungumzuia maandalizi ya Mkutano wa 27 wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) unaotarajiwa kufanyika nchini Misri Novemba mwaka huu.
Dkt. Jafo alisema hii ni heshima kubwa kwa Bara la Afrika kushiriki katika mkutano huo na kwamba ushiriki wa Tanzania utatoa fursa katika kutangaza namna inavyoshirikiana na wadau katika hifadhi ya mazingira.
“Nikiri wazi ushiriki wetu kule Misri utakuwa mzuri na mpana na tayari tumeanza kufanya maandalizi ya ushiriki tukiwa taasisi zetu na wadau wegine ambapo tunatarajia kuonesha kazi zetu kupitia mkutano huo," alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kusukuma ajenda ya kuzitaka nchi zinazoendelea kutoa fedha barani Afrika kwa ajili ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Balozi Mhe. Abulwafa alisema nchi yake inatarajia Tanzania itanufaika na COP27 kwa vile ni mojawapo ya nchi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, alipongeza jitihada zinazofanywa na Tanzania katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.