Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa mataifa duniani kushirikiana katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ametoa wito huo leo wakati akifungua Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ulioandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza na kushirikisha zaidi ya nchi 20 duniani.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Dkt. Jafo alisema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani inakabaliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema changamoto hizo zinaathiri uzalishaji wa chakula unaosababishwa na ukame na mafuriko ya kudumu, uharibifu wa miundombinu, uharibifu wa ardhi, uchakavu wa vyanzo vya maji, upotevu wa maji. ya viumbe hai, viumbe vamizi, uhamiaji na mlipuko wa magonjwa.
Hivyo, Waziri Jafo alisema kutokana na athari hizo, Tanzania inatumia wastani wa Dola za Kimarekani milioni 500 kwa mwaka katika kuchukua hatua za kukabiliana na hali hiyo.
“Katika mkutano tutaweza kujadiliana na wenzetu kutoka mataifa mbalimbali duniani kuhusu changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na namna ya kupata fedha zitakazotumika katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
Aidha, Dkt. Jafo alibainisha kuwa Tanzania iliazimia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kati ya asilimia 30 hadi 35 ikilinganishwa na mazingira ya biashara ya hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2030, ambapo takriban tani milioni 138 hadi 153 za hewa hiyo zinatarajiwa kupungua.
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza, Mhe. David Concar alisema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuzikutanisha nchi mbalimbali kujadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Concar alisema kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kuwa nchi zinazoendelea kuchangia katika mapambano haya ya mabadiliko ya tabianchi katika Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) uliofanyika Glasgow, Scotland ni wakati sasa wa kutekeleza maazimio hayo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dkt. Omar Dadi Shajak alisema maeneo 143 ya Visiwa vya Zanzibar yameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kwa kuingiliwa na majichumvi kutoka baharini.
Alisema kutokana na changamoto hiyo, kilimo cha mpunga kimeathiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi hali iliyosababisha uzalishaji wa mpunga kupungua kwa kiasi kikubwa.
Hivyo, Dkt. Shajak alisema mkutano huo utasaidia kuweka mikakati endelevu ikiwemo kutafuta njia mbadala wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.