[caption id="attachment_43159" align="aligncenter" width="900"] Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia afya Dkt Dorothy Gwajima akizungumza na wajumbe wa kamati ya uendeshaji afya ya Mkoa wa Singida wakati alipofanya ziara katika wilaya ya Manyoni leo.[/caption]
Na Angela Msimbira Singida
Naibu Katibu Mkuu Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Dorothy Gwajima, amewaondoa katika uongozi wajumbe wanane wa timu ya uendeshaji na usimamizi wa huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida kwa kushindwa kuwajibika kikamilifu katika kutekeleza wajibu wao wa msingi.
Akiwa kwenye ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida kukagua utendaji kazi wa watoa huduma za afya Mkoani hapo leo Dkt Gwajima amewataka waendelee na majukumu yao ya kitaaluma kwa mujibu wa ajira zao badala ya majukumu ya uongozi hadi hapo itakapoelekezwa vinginevyo.
Dkt. Gwajima amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Victorina Ludovick kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuteua timu ya mpito hadi hapo uchambuzi wa kina cha uzembe utakapofanyika kwa ajili ya hatua zaidi.
[caption id="attachment_43160" align="aligncenter" width="900"] Baadhi ya wajumbe wa kamati ya uendeshaji afya ya wilaya ya Manyoni na Mkoa wa Singida wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt Dorothy Gwajima leo mjini Manyoni.[/caption]Ameagiza timu iliyopumzishwa majukumu ya uongozi kutoa maelezo ndani ya siku 7 kwanini walishindwa kusimamia kikamilifu utendaji kazi wa kituo hicho na kwa nini wasivuliwe majukumu ya uongozi jumla.
Vilevile, amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida na timu yake nao kutoa maelezo kwa nini wameshindwa kubaini uzembe wa uwajibikaji wa timu ya usimamizi na uendeshaji huduma wa Halmashauri ya Wilaya hiyo na kwa nini nao wasiwe sehemu ya kuchangia tatizo.
Dkt. Gwajima ameitaka timu ya afya Mkoa kutoondoka Manyoni hadi changamoto zote zinazohitaji hatua za haraka zifanyiwe kazi na watoe taarifa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo itarejea kwa ukaguzi wa kina katika Halmashauri hiyo.
Aidha, Dkt Gwajima amewapongeza watoa huduma walioko mawodini kwa kujituma katika kuhudumia wagonjwa.