Na Mathew Kwembe, Babati
Serikali imezitaka Halmashauri za Wilaya kuhakikisha kuwa zinatekeleza agizo lake la kuhakikisha wanaimarisha upatikanaji wa dawa katika vituo vya huduma za afya na kuepuka tabia ya kuwaandikia wagonjwa kwenda kununua dawa nje ya kituo.
Agizo hilo limetolewa jana mjini Babati na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt Dorothy Gwajima mara baada ya kuitembelea hospitali ya Mrara ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kukagua huduma za afya na uwezo wa timu za usimamizi huduma za afya mikoa na halmashauri.
Amesema, kila halmashauri haina budi kutenga fedha toka vyanzo vya ndani kwa ajili ya kuhakikisha dawa zilizokosekana bohari kuu ya dawa zinanunuliwa na stoo za dawa katika hospitali zinakuwa na dawa aina zote muda wote ili kuepuka kuwaandikia wateja kwenda kununua dawa hizo nje ya maduka ya hospitali.
“Hivi halmashauri zinashindwa nini kutenga fedha toka vyanzo vya ndani kwa ajili ya kuandaa chumba maalumu cha kutunza dawa kisha kununua dawa aina zote kufidia zilizokosekana bohari kuu ya dawa ili, wateja wanaoelekezwa kununua nje ya hospitali wapate dawa hizo ndani ya hospitali husika, mbona maelekezo haya kwingine yamewezekana nyie mnagonja nini?” amehoji Dkt. Gwajima. Kauli hiyo ya Dkt Gwajima inafuatia maelezo ya Mfamasia wa Hospitali ya mji bwana Elly John Bomani kwamba baadhi ya dawa muhimu katika hospitali hiyo zinakosekana ambapo juhudi za kuagiza dawa nyingine bohari kuu ya dawa zimekwishafanyika. Akizungumzia kuhusu hali ya utoaji wa huduma aliyoikuta kwenye hospitali hiyo, Dkt Gwajima ameelezea kutofurahishwa na hali ya usafi wa mazingira na kuelekeza mganga mkuu wa mkoa asimamie usafi wa kina ufanyike vilevile, waganga wakuu wa mikoa na halmashauri zote waelekeze macho yao kwenye usafi wa mazingira kila eneo la huduma na asikute tena popote hali ya usafi wenye mashaka. “Sitarajii nikute haya mambo madogo kabisa hayaridhishi, natarajia nikute hoja kubwa za kimkakati ili, tujadiliane hizo. Hii habari ya kukutana na magodoro yaliyochoka hayana mipara stahiki ya kufunika, viti vimechoka, vyoo na bafu zisizofanyiwa usafi, vumbi, mara milango na madirisha yako wazi hapana kabisa. Naagiza mapungufu haya yafanyiwe kazi mara moja na magodoro yaliyochoka yachambuliwe yatolewe na mganga mkuu wa mkoa uniletee taarifa,” amesema. Hivyo Dkt Gwajima amemwagiza Katibu wa Afya wa Mkoa Bwana Thomas Malle kuhakikisha kuwa anatekeleza wajibu wake wa kusimamia kikamilifu wataalamu wa afya ya mazingira wa halmashauri wahakikishe kuwa usafi unafanyika katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika mkoa wa Manyara ama la sivyo naye ajipime maana yuko karibu kabisa na hospitali hiyo
“Mimi nashangazwa inakuwaje timu ya usimamizi huduma za afya halmashauri ofisi zake ziko humu humu hospitalini lakini hali ya kituo ni hivi, na mwaka mzima hawajafanya ukaguzi, huu ni utendaji wa mazoea, naenda kutakafari juu yenu,” amesema Dkt Gwajima.
Ameongeza “Sitaki mazoea wala wasaidizi ambao inabidi nitumie nguvu kubwa kuwafanya watekeleze majukumu yao ya msingi bali kila mmoja ajitume mwenyewe vinginevyo ama akabidhi kwa hiari madaraka aliyopewa ama kwa lazima.”
Pia Naibu Katibu Mkuu ametembelea jengo la Maabara na kukuta kuwa hospitali hiyo haitoi baadhi ya huduma za vipimo muhimu huku, mashine kwa ajili ya vipimo hivyo zipo na wataalamu wapo.
Dkt Gwajima ametaja vipimo hivyo kuwa ni culture and sensitivity ambapo, sababu iliyotolewa ni kuwa, wako kwenye mchakato wa kukarabati jengo huku makadirio ya gharama yakiwa ni madogo na yapo ndani ya uwezo wa hospitali.
Naibu Katibu Mkuu amemuagiza Mganga mkuu wa mkoa aifuatilie timu ya usimamizi huduma za afya ya halmashauri ya mji wa Babati ili iachane na habari ya neno mchakato na badala yake watumie utaratibu wa force account kununua vifaa na kutumia mafundi wa kutoka jamii wafanye kazi hiyo na ndani ya siku 30 watoe taarifa ya kuwa zoezi limekamilika.
“Maeneo mengi nilikopita naona baadhi ya wasaidizi wangu hawajaielewa kasi tunayotakiwa kwenda nayo kwa kuwa naendelea kushuhudia mambo madogo madogo yakiwa hayajatekelezwa kinyume na maelekezo na makubaliano tuliyojiwekea na mambo haya wala hayahitaji fedha wala si kwamba, wasaidizi wangu wamezidiwa na majukumu, ni mazoea tu,” amesema
Dkt Gwajima amehoji: “Hivi huwa mnakuwa mnafanya nini kila siku hadi kunakuwa na mapungufu kama haya na wengine mnalalamikiwa kwa tuhuma za wizi, rushwa, ubadhirifu na lugha chafu kwa wagonjwa?”
Katika ziara hiyo Dkt Gwajima aliambatana na kamati ya usimamizi huduma za afya ya halmashauri ya mji wa Babati pamoja na ile ya Mkoa wa Manyara ambapo amemtaka Mganga mkuu wa mkoa kuongeza kasi ya kusimamia timu za halmashauri na kujiridhisha kama wasaidizi wake wanamsadia au nao ni sehemu ya wanaohitaji kutazamwa upya.
Wakati huo huo Dkt Gwajima amewataka Makatibu wa Afya wa Mikoa, Wilaya na Vituo vya kutolea huduma za afya kuandaa kanuni na taratibu za taasisi (organizational culture) zitakazowaongoza watoa huduma kufikia uwajibikaji bora zaidi.
Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu alimpongeza Dkt Pastory Mahendeka ambaye ni daktari wa meno wa hospitali ya mji wa Babati kwa kufanya majukumu yote ya ujumbe wa timu ya usimamizi wa huduma za afya halmashauri na pia kumudu kufanya majukumu ya kitabibu na kuandaa takwimu zake vizuri bila kusimamiwa wala kufuatiliwa.
Amemuelekeza kuwa, kwa kuwa yuko peke yake, vema aweke kwenye mpango utaratibu wa kuomba kibali cha watumishi wengine kupelekwa masomoni.
Vilevile, Naibu Katibu Mkuu amepongeza daktari wa wodi ya watoto kaika hospitali ya mji wa Babati Dkt. Moses Mollel kwa uwajibikaji wake makini katika kutoa huduma za kitabibu katika wodi hiyo kila siku na kwa kumbukumbu zisizotia shaka.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt Damas Kayera amesema wamepokea maagizo ya Naibu Katibu Mkuu na akaahidi kuyatekeleza kikamilifu na kuendeleza ufuatiliaji kama huu katika halamshauri zingine.
Naye Mratibu wa Malaria kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi Stellah Kajange ameutaka uongozi wa hospitali ya mji wa Babati kuhakikisha kuwa inajenga kichomea taka cha kisasa kwani kilichopo sasa hakifai.
Naibu Katibu Mkuu pia ametembelea kituo cha afya Magugu kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati, ambapo ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Babati kwa kusimamia vema ujenzi wa jengo la huduma za uzazi na upasuaji na kuwataka huduma zianze kutolewa kwenye jengo hilo ifikapo tarehe 10 Juni, 2019.
Naibu Katibu Mkuu alikuwa kwenye ziara ya siku mbili kutembelea vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Manyara.