Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Biteko Atoa Kompyuta 10 Shule ya Sekondari Rusumo B
Sep 29, 2023
Dkt. Biteko Atoa Kompyuta 10 Shule ya Sekondari Rusumo B
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza leo Septemba 29, 2023 na wananchi (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Shule ya Sekondari Rusumo B kupitia mradi wa REA III, mzunguko wa Pili katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.
Na Lilian Lundo na Veronica Simba

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa kompyuta 10 kwa Shule ya Sekondari Rusumo B mara baada ya kuwasha umeme shuleni hapo.

Mhe. Dkt. Biteko ametoa kompyuta hizo leo Septemba 29, 2023 wakati wa hafla ya kuwasha umeme shuleni hapo kupitia mradi wa REA III, mzunguko wa Pili katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.

“Tuanzishe madarasa ya kompyuta, tutawatafutia kompyuta 10 kwa ajili ya wanafunzi wetu, tunafanya kila kinachowezekana msiishi maisha tuliyoishi,” amesema Mhe. Dkt. Biteko.

Aidha, amewataka wanafunzi hao kuwa na nidhamu na juhudi katika masomo yao, ili waweze kufikia malengo ambayo wamejiwekea.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Rusumo B, Mwalimu Geze John amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa  kuwezesha shule  hiyo kupata umeme, hivyo kuondokana na changamoto ya umeme wa Sola iliyokuwa ikitumika.

Amesema umeme wa Sola waliokuwa wakiutumia ulikuwa na changamoto, ikiwemo kutoa mwanga hafifu ambao ulikuwa unahatarisha uoni wa wanafunzi, vilevile ulikuwa hauwezi kutumika kwa muda mrefu, hivyo wanafunzi walikuwa wakisoma kwa muda mfupi wakati wa usiku.

Vilevile amemshukuru Mhe. Dkt. Biteko kwa kuwapatia kompyuta 10 na amesema tayari walikuwa na mwalimu wa kompyuta, hivyo kompyuta hizo zimekuja wakati muafaka ambapo tayari wamewawashia umeme wa REA.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi