Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi ametoa wiki moja kwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo kuitisha kikao na vyama vyote vya michezo vilivyopo kwenye mgawanyo wa wachezaji (Quarter) kwenye Mashindano ya Madola yatakayofanyika Julai 2022 nchini Uingereza ili kusikiliza changamoto na kuwapa mwelekeo wa namna bora ya usimamizi wa michezo kuelekea mashindano ya kimataifa.
Dkt. Abbasi ametoa maelekezo hayo leo kwenye kikao alichokiitisha Disemba 3, 2021 kilichoshirikisha Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Baraza la Michezo la Taifa, Baraza la Michezo la Majeshi na Kamati ya Olympic ya Tanzania (TOC) ili kupokea taarifa ya TOC na Mpango kazi wa maandalizi ya timu za taifa kuelekea maandalizi ya ushiriki wa Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Aidha, wajumbe wameiomba Serikali kutupia macho kwenye baadhi ya vyama vya michezo visivyofuata utawala bora ili kuwafanya wachezaji kufanya vizuri.
Akizungumzia maendeleo ya michezo nchini, amesema kwa sasa ni muhimu kuchagua michezo michache ya kimkakati inayofanya vizuri ili kupata mafanikio.
Aidha, Dkt. Abbasi amefafanua kwamba ili kuendeleza michezo nchini ni muhimu kwa wadau hao kubuni vyanzo vya uhakika mapato vitakavyotoa fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli za michezo.
“Tunatarajia kuanza makambi ya michezo mapema ili kujiandaa na michezo ya kimataifa”, amesisitiza Dkt. Abbasi.