Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Abbasi Atoa Ofa kwa Vikundi vya Utamaduni, Afunga Tamasha la Cigogo
Jul 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Shamimu Nyaki - WUSM

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amefunga Tamasha la 13 la Muziki wa Cigogo kwa kutoa ofa kwa vikundi vitatu vilivyoshiriki Tamasha hilo kupata nafasi katika matamasha makubwa yajayo.

Dkt. Abbasi ametoa ofa hiyo Julai 24, 2022 katika Viwanja vya Chamwino Arts Center ambapo amesema Agosti 21, 2022 kutakuwa na Tamasha kubwa la kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, maarufu #SensaBika, ambapo amesema kikundi kimoja kitashiriki kwa gharama za wizara na kupata nafasi ya kwanza kutoa burudani.

"Tarehe 26, Agosti 2022, kutakua na Tamasha la ‘Tanzania and India Cultural Event’ ambalo tutalifanya kwa kushirikiana na wenzetu wa India, hapa natoa ofa tena Kwa kikundi kimoja kuwa miongoni mwa vikundi vitakavyoshiriki katika tamasha hilo", aliongeza Dkt. Abbasi

Ametaja ofa nyingine kuwa, katika Tamasha la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo litakalofanyika mwezi Oktoba 2022 Bagamoyo, kikundi kimoja kitashiriki kuonesha utamaduni wao.

Aidha, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa, wizara hiyo chini ya Waziri, Mhe. Mchengerwa inaendelea kufanya mageuzi katika Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo Sekta hizo zimeendelea kuitangaza nchi ya Tanzania duniani, huku akisisitiza kuwa itaendelea kuupiga mwingi zaidi.

Dkt. Abbasi ametumia nafasi hiyo, kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika nchini Agosti 23, 2022.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa, Dkt. Kedmon Mapana ambaye pia ni Mwanzilishi wa Tamasha hilo, ameishukuru wizara kwa kuunga mkono tamasha hilo na kuahidi kuliboresha zaidi.

Tamasha hilo lilianza Julai 22 hadi 24, 2022, liliongozwa na Kauli Mbiu "Elimu ya Sanaa ni Muhimu kwa Maendeleo Endelevu".

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi