Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi akiongea wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo maalum kuhusu uandishi wa habari za usalama barabarani leo jijini Dar es Salaam (Picha na MAELEZO)
Na Mwandishi wetu, MAELEZO
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amewataka waandishiwa habari nchini kutumia taaluma ya habari kuielemisha jamii juu ya usalama barabarini ili kupunguza ajali ambazo zimeendelea kusababisha vifo visivyo vya lazima na ulemavu wa maisha.
Dkt. Abbasi ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi mafunzo maalumu ya miezi sita juu ya uandishi bora wa habari zinazohusu usalama barabarani, kwa waandishi wa habari 17 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Ameeleza kuwa ajali za barabarani zitapungua kwa kiwango kikubwa endapo waandishi wa habari watatumia taaluma yao kuielemisha jamii juu ya usalama barababrani, kupaza sauti za wananchi pale palipo na changamoto zinazohitaji usimamizi wa Serikali na pia kuwa sehemu ya mageuzi yanayofanywa na Serikali kuwaondolea wananchi changamoto za ajali.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali akimkabidhi vitendea kazi mwandishi wa Gazeti la Habarileo, Evance Ng'ingo ambaye anashiriki mafunzo maalum ya miezi sita kuhusu usalama barabarani (Picha na MAELEZO)
“Zaidi ya watu milioni moja na laki mbili hufariki kila mwaka duniani kutokana na ajali za barabarani na kati ya vifo hivyo asilimia 90 hutokea katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania. Wengi wanaofariki kwa ajali ni watu wenye umri wa kati ya miaka 15-29 na hivyo kuwa na atahari kubwa kiuchumi na kijamii,” alieleza Dkt. Abbasi.
Amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia kwa umakini mafunzo watakayopata ili watumie maarifa watakayoyapata kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na wadau wa usalama barabarani.
Nae Mkurugenzi wa Uhakiki na Ubora kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Mohamed Mohamed, amesema kuwa Wizara pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) wameona ni muhimu waandishi wa habari kuwa na ufahamu wa kutosha juu ya masuala ya usalama barabarani kwa kuwa wao wana nafasi kubwa ya kufikisha elimu hiyo kwa jamii kubwa zaidi.
Dkt. Mohamed ameeleza kuwa watu wengi wamekuwa wakipoteza maisha katika ajali kutokana na sababu nyingi ikiwemo majeruhi kukosa huduma za haraka pindi ajali inapotokea kutokana na hospitali kuwa mbali.
Amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto ya majeruhi kukosa huduma za haraka wakati wa ajali, Wizara ipo katika hatua za mwisho kuweka vituo vya kutolea huduma za dharua (Emergency Medicine Services Centre) katika barabarani kuu ziendazo mikoani ambapo vitarahisisha kuwapatia huduma za haraka majeruhi wa ajali.
Baadhi ya wadau wa habari walioshiriki uzinduzi wa mafunzo ya usalama barabarani kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam. (Picha na MAELEZO)
Waandishi wanaoshiriki mafunzo haya ni pamoja na Abadallah Msuya kutoka Daily News, Evance Ng’ingo na Adam Ruta kutoka Habarileo, Agness Mbapu kutoka TBC, Beaty Tesha kutoka TBC Taifa, Aisia Rweyemamu na Chrispin Gerald kutoka The Guardian, Dickson Kanyika kutoka Star Tv na Radio Free Africa, Herrieth Makweta kutoka Mwananchi na Jasmin Shamweku kutoka Redio ABM ya Dodoma.
Waandishi wengine ni Juhudi Felix kutoka FADECO Wilayani Karagwe, Margaret Malisa kutoka Nipashe, Renatus Mutabuzi kutoka ITV, Sylvanus Kayela kutoma Mlimani TV, Veronica Mrema kutoka Mtanzania na Vumilia Kondo kutoka Abood Media ya Morogoro.
Mafunzo haya usalama barabarani kwa waandishi wa habari ni ya tangu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016 kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Shirika la Afya Duniani.