Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) kukabidhi eneo la Kilomita za mraba 25,000 kutoka kwenye Hifadhi
ya Msitu wa Morogoro unaosimamiwa na wakala huyo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za
Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Ametoa agizo hilo jana akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Morogoro ambapo alimuagiza Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo, Mej. Jen. Gaudence Milanzi kuzikutanisha taasisi hizo ndani ya
siku saba zijazo ili kukamilisha mchakato wa kumega eneo hilo na kukabidhiwa
kwa Mamlaka hiyo ili taratibu za ujenzi ziweze kuanza.
Aidha, ameuagiza uongozi huo wa TFS kuweka vigingi vya mpaka katika eneo la hifadhi hiyo ya msitu ndani ya
siku 30 zijazo huku akitoa muda huo kwa wananchi wote waliovamia eneo hilo kuondoka
mara moja kwa hiari yao wenyewe kabla ya kuondolewa kwa nguvu.
Katika hatua nyingine, Dk.Kigwangalla amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo, Prof. Dos Santos Silayo kukabidhi
mbao zaidi ya 400 zilizokamatwa hivi karibuni mkoani Morogoro baada kuvunwa
kinyume cha Sheria kwa uongozi wa Mkoa huo ili zisaidie kutengeneza madawati ya
shule za msingi.
Pamoja na mbao hizo amemuagiza pia mtendaji huyo kukabidhi kwa uongozi wa mkoa huo magunia 350 ya mkaa yaliyokamatwa
katika kituo cha TAZARA yakiwa yanasafirishwa kinyume cha Sheria ili yasambazwe
kwenye shule za Sekondari mkoani humo.
Dk. Kigwangalla alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro
inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Steven Kebwe, ambapo alimuomba kusimamia
zoezi hilo la ugawaji kikamilifu ili walengwa waweze kufikiwa.