Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla ameteua Kamati maalum ambayo itaishahuri Serikali namna ya nini kifanyike katika kushughulikia athari za bonde la Kilombero lililopo Mkoani Morogoro.
Waziri Dk Kigwangalla amebainisha kuwa kamati hiyo aliyoiteua ndio itakayomshauri juu ya bonde hilo litasimamiwa vipi pamoja na namna bora ya hatua za kuchukua ili kulinda bonde hilo ambalo lina mahitaji makubwa ikiwemo chanzo kikubwa cha maji yanayotengeneza Stiegler’s Gorge na kuwepo na aina zaidi ya 400 ya ndege pamoja na mnyama aina ya Puku ama Sheshe ambaye hapatikani Duniani kote zaidi ya Tanzania pekee.
"Hii ndio Kamati yangu itakayonishahuri juu ya bonde ili litasimamiwa vipi. Hii ndio Kamati ambayo itanishahuri mimi na Serikali kwa ujumla wake juu ya namna bora ya uhifadhi hususani katika eneo lile la Pori tengefu”,alisema Kigwangalla.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe mbalimbali ambao wataongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Ndugu Andrew Napacho, pia wajumbe ni Brig. Gen. (Mst.) Edmund Mndolwa, aliyekuwa Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Mstaafu, Suleiman Kova, Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha wafugaji Bwana Semkae Kilonzo (Policy Forum).
Wengine ni Dk. Simon Mduma, Prof. Jaffar Kideghesho, Ruzika Muheto, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, MKuu wa Wilaya ya Kilombero, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mwenyekiti Halmashauri Ulanga, M/Halmashauri Kilombero, M/Halmashauri Malinyi na M/Halmashauri Ifakara.
Pia yupo Mtendaji Mkuu wa KPL, Mtendaji MKuu wa Illovo, Mkuu Kikosi JKT Chita. Wengine ni Dk. Aggrey Mlimuka, Mwakilishi kutoka mamlaka ya maji Bonde la Kilombero, Mwakilishi kutoka Wizara ya ardhi.
Wajumbe wengine ni Ndugu. Innocent Kylogeris, Dk. James Wakibara pamoja na Mkurugenzi Mkuu TAWA ambaye atakuwa Katibu wa Kamati hiyo.
Hatua hiyo inafuatia Waziri Dk Kigwangalla kufanya ziara maalum kwenye bonde hilo la kilombero ambapo ameweza kushuhudia athari kubwa zaidi zilizofanywa na wavamizi wakiwemo wakulima na wafugaji ambao wameonekana kuvamia maeneo makubwa ndani ya pori tengefu la bonde pamoja na Kwenye eneo ohevu ndani ya bonde hilo.