Na ; Mwandishi wetu- Uyui
Viongozi wa Wilaya ya Uyui wametakiwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zinazochangiwa na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata zote za Wilaya hiyo.
Akizungumza katika Kijiji cha Songambele kilichopo Kata ya Miyenze, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Gift Issaya Msuya amesema kuwa wananchi wanayohaki ya kujua mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo wanayochangia ili kuongeza tija katika kutekeleza miradi hiyo.
"Kuanzia sasa mimi niko Wilaya ya Uyui nisije nikasikia kwamba mnafanya mambo bila ya kuwashirikisha wananchi, mmechangisha michango, mmeanza kutekeleza miradi ya maendeleo ni lazima muwashirikishe wananchi kwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi na kila hatua inayofikiwa katika utekelezaji wa mradi husika"; Alisisitiza Msuya.
Akifafanua amesema kuwa wananchi wanapaswa kupata taarifa ya kila jambo katika maeneo yao na huo ndio utawala Bora unaosisitiza uwazi na uwajibikaji kwa wananchi.
Agizo hilo litaongeza kasi ya maendeleo katika Kata zote za Wilaya hiyo na hivyo kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza Viongozi kuwajibika katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Miyenze Samweli Manyika ameahidi kuwa watafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo wakati wa ziara yake katika Kata hiyo iliyolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika miradi ya maendeleo katika maeneo yao hasa kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji.
Aliongeza kuwa wataongeza kasi yakutoa taarifa kwa wananchi kuhusu miradi ya maendeleo ambayo wananchi wamekuwa wakichangia fedha na rasilimali mbalimbali ili kuchochea maendeleo katika maeneo yao.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele Bw. Shaban Mingili amesema kuwa atasismamia utekelezaji wa agizo hilo la kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo kama ilivyoagizwa.
Mkuu wa Wilaya ya Uyui amekuwa akisisitiza uwazi na uwajibikaji kwa viongozi wa katika ngazi zote katika Wilaya hiyo ili kuendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza uwazi na uwajibikaji katika kuwaletea wananchi maendeleo.