[caption id="attachment_39338" align="aligncenter" width="341"] Mkuu wa Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora Mhe Gift Isaya Msuya[/caption]
Na ; Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora Mhe. Gift Isaya Msuya amesema kuwa Wilaya hiyo imejipanga kutekeleza miradi ya kimkakati itakayosaidia kuwakwamua wananchi kiuchumi katika kipindi cha mwaka 2019.
Akizungumza katika mahojiano maalum amesema kuwa miradi hiyo itajikita katika sekta za Kilimo, Ufugaji, Elimu, Afya ambapo itawawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi na kujiletea maendeleo .
“ Tumelenga kujenga Mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa Wilaya yetu ina ardhi yenye rutuba na wananchi wanao uwezo mkubwa wa kushiriki katika uzalishaji kupitia sekta hii ndio maana tumeamua kuweka mikakati ya kukuza uzalishaji na kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda”. Alisisitiza Mhe. Msuya
Akifafanua amesema kuwa kilimo cha umwagiliaji kitasaidia kuongeza uzalishaji wa mpunga pamoja na mazao mengine ya biashara yatakayochochea ustawi wa wananchi na kukuza uchumi kwa ujumla.Akizungumzia huduma za afya amesema kuwa Wilaya hiyo imepokea shilingi Bilioni moja na nusu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo na tayari maandalizi ya ujenzi yameanza ambapo mradi huo utakapokamilika utakuwa ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo na maeneo ya jirani.
Alitaja miradi mingine inayotekelezwa katika Wilaya hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha Afya katika jimbo la Igalula kilichogharimu milioni 400 ambapo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho kukamilika ili wananchi waanze kupata huduma.
Kwa upande wa kituo cha Afya Utege kilichopo jimbo la Tabora Kaskazini Mhe. Msuya amebainisha kuwa kimekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo hali inayoonesha dhamira safi ya Serikali kuleta ustawi kwa wananchi kwa kuboresha huduma za afya.“ Upatikanaji wa dawa katika Wilaya yetu kwa sasa umefikia asimilia 95 hivyo nachukua fursa hii kumpongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali wananchi wanyonge kupitia huduma hizi muhimu zinazolenga kuleta ustawi kwa wananchi na Taifa kwa ujumla”. Alisisitiza Msuya.
Akisisitiza kuhusu maendeleo katika Wilaya hiyo Msuya amesema kuwa Wilaya hiyo imejipanga kuhakikisha kuwa miradi yote iliyopangwa inakamilika kwa wakati ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, miradi ya maji iliyokwama kwa muda mrefu ili kuongeza kasi ya maendeleo .
Eneo jingine litakalopewa kipaumbe katika sekta ya elimu ni ujenzi wa mabweni katika Kata 15 Wilayani humo ili kuchochea maendeleo ya sekta ya elimu kwa kuwajengea wasichana mazingira rafiki katika shule wanazosoma hali itakayochangia ukuaji wa kiwango cha elimu kupitia kampeni ya ” Nishike Mkono Kuboresha Elimu Uyui” iliyoanzishwa na mkuu wa Wilaya hiyo mara baada ya kuteuliwa.
Kata zitakazonufaika na ujenzi wa mabweni ni ; Magiri, Igalula, Gaweko, Tura, Usagari, Ilolangulu, Mabama, Kizengi, Lutende, Shitage, Loya, Upuge, Ikongolo na Makazi.Pia aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia katika kampeni ya ”Nishike Mkono Kuboresha Elimu Uyui” ili kuchangia katika kuinua kiwango cha elimu katika Wilaya hiyo kwa kujenga mazingira rafiki kwa watoto wa kike kupitia ujenzi wa mabweni hayo.
“Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa mwaka 2019 ni pamoja na ujenzi wa stendi mpya na eneo la maegesho ya magari makubwa”. Alisisitiza Mhe Msuya.
Alitaja baadhi ya faida za miradi hiyo kuwa ni pamoja na kuchangia katika kukuza uchumi wa Wilaya hiyo kwa kuzalisha ajira.Aidha; Mhe Msuya alipongeza utaratibu wa kuwapatia Wajasiriamali wadogo maarufu kama wamachinga vitambulisho maalum vinavyowawezesha kutekeleza majukumu yao bila kubugudhiwa na pia kuchangia katika ujenzi wa uchumi.
Wilaya ya Uyui ni moja ya Wilaya za mkoa wa Tabora ambayo ina ardhi yenye rutuba, misitu na inatarajia kuwainua wananchi wake kiuchumi kupitia mikakati mbalimbali iliyowekwa na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Watendaji wengine ikilenga kuchochea maendeleo.