Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DC Tabora: Jengeni Utaratibu wa Kutunza Kumbukumbu za Biashara Kuepuka Matumizi Yanayoleta Hasara
Oct 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent, RS- TABORA

SERIKALI ya Wilaya ya Tabora imetoa wito kwa wajasiriamali kuwa utaratibu wa kutunza kumbukumbu za matumizi ya fedha katika biashara zao ili zidumu na ziwe endelevu hatimaye kuepuka hasara zinazoweza kuepukika kutokana na matumizi yasiyo ya lazima.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Queen Mlozi wakati akifungua  Jukwaa la Biashara la NMB (NMB Business Club) kwa wajasirimali 200 kutoka Tabora.

Alisema kuwa elimu kuhusu  utunzaji wa kumbukumbu za biashara , masoko , huduma nzuri kwa mteja , upangaji bei , sheria za biashara, ulipaji wa kodi ni muhimu kwa wafanyabiashara wengi kufanya shughuli zao kwa tija na faida

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa mafunzo yaliyotolewa na Benki ya NMB kwa wajasiriamali kuhusu umuhimu wa ulipaji wa kodi na utunzaji wa kumbukumbu za fedha yatawajenga uwezo wao juu ya ulipaji kodi kwa hiari na kuepuka vitendo vya ukwepaji kodi.

Alisema kuwa ili wajasiriamali hao wafanikiwe ni lazima wajenge nidhamu katika matumizi na kuelekeza fedha zao katika maeneo muhimu na kisha kuwa na kumbukumbu ya jinsi walivyotumia fedha hizo

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliongeza kuwa Kodi ni muhimu katika kuchochea maendeleo na uwekaji wa miundo mbinu mizuri na mazingira wezeshi kwa Serikali katika kuwaletea wananchi na  wajasiriamali kushiriki katika mbalimbali za maendeleo.

Queen alisema kuwa mafunzo hayo yatawapa sauti moja wajasiriamali kupitia Jukwaa hilo ili kujenga mahusiano na Taasisi nyingine kwa ajili ya kuboresha baishara wanazozifanya kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Alitoa wito kwa wajasiriamali hao kutumia elimu hiyo katika kuhakikisha kuwa wanaendesha baishara zao kwa kuzingatia taratibu na sheria ili biashara zao ziweze kukuwa na kuleta tija kwao na Taifa kwa ujumla.

Meneja wa Kanda ya Magharibi wa Benki ya NMB Leon Ngowi alisema kuwa Jukwaa hilo ni fursa ya kukutana na wadau wao na 430 litawasadia kupata mrejesho kutoka kwa wadau wao kwa ajili ya kuboresha huduma zao.

Alisema kuwa pia watawapa mbinu mpya za kuendesha biashara zao ikiwa ni pamoja na njia nzuri za utunzaji wa kumbukumbu za hesabu zao na kutengeneza mipango ya biashara zao ili ziwe na tija na endelevu.

Naye Mkufunzi kuhusu Elimu ya Biashara kutoka Agriculture and Finance Consultants Erick Chrispin akitoa mada inayohusu jinsi ya kuendesha biashara katika mdororo wa uchumi alisema kuwa wafanyabiasha ni vema wakajenga utaratibu wa kuwa na mafaili  sita katika kazi zao ili kufanyabiashara yao kuwa endelevu.

Alitaja mafaili hayo ni kuwa ya mauzo, manunuzi, gharama, nyaraka za kodi, nyaraka za Benki na mikataba ya kiashara.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi