Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DAWASCO imejipanga kuongeza usambazaji wa maji safi Dar es salaam
Oct 17, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA

Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) limejipanga kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama jijini Dar es salaam ifikapo June mwaka 2018.

Akizungumza katika kipindi maalumu cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC), Afisa Mtendaji Mkuu DAWASCO Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kuwa takribani shilingi bilioni 114 zimepatikana kutoka benki ya dunia ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu na zitatumika kuboresha miundombinu ya maji katika jiji la Dar es salaam.

"Kwa sasa DAWASCO inazalisha lita milioni 510 za maji ambapo mpaka sasa Shirika limewaunganisha wananchi wa kawaida 25,000 wanaolipa kwa awamu na kuendelea kuunganisha wateja wapya” amesema Mhandisi Luhejema.

Aidha, Mhandisi Luhemeja ameishukuru Serikali hasa katika kipindi hiki cha miaka miwili kuiwezesha DAWASCO kusambaza huduma ya maji kutoka asilimia 67 hadi asilimia 75 ikiwa na lengo la kufika asilimia 95 mwaka 2020.

“Tunataka kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa maji na kwa ushirikiano tunaoupata kwa sasa tutahakikisha tunatatua changamoto ya upatikanaji wa maji ili huduma hii muhimu iweze kuwafikia wakazi wengi zaidi katika maeneo tunayohudumia." Alisema Mhandisi Luhemeja.

Vilevile Mhandisi Luhejema ameongeza kuwa DAWASCO ina visima 32 vya maji vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya jijini Dar es salaam na mabwawa tisa kwa ajili ya kusafisha maji ikiwa mabwawa yenye takribani kilometa 300 yaliyopo katikati ya jiji.

Mbali na hayo, Mhandisi Luhemeja amesema kuwa DAWASCO inashirikiana na Mamlaka ya Maji safi na maji taka Dar es salaam (DAWASA) katika kuhakikisha kuwa visima vya Kimbiji na Mpera vinakamilika na kuanza kuzalisha maji kwa wakati.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi