Na; Frank Mvungi
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA)imejiwekea malengo ya kukusanya shilingi bilioni 12 kila mwezi ikiwa ni sehemu ya matokeo ya maboresho yanayofanyika ili kuongeza tija katika huduma zinazotolewa na Mamlaka hiyo.
Akizungumza katika Kipindi cha “TUNATEKELEZA” kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC),Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanafikiwa na huduma ya majisafi na salama katika maeneo yote hapa nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake.
“Kuunganishwa kwa DAWASCO na DAWASA kunalenga kuongeza tija katika huduma zinazotolewa kwa wananchi na kupunguza gharama za uendeshaji hali itakayosadia fedha zinazookolewa kuelekezwa kuboresha huduma kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni”. Alisisistiza Mhe. Prof. Mbarawa
Akifafanua amesema kuwa asilimia 35 ya mapato yote ya DAWASA yanayokusanywa yataelekezwa katika kupeleka huduma ya maji kwa wananchi walio maeneo ya pembezoni.
Aliongeza kuwa DAWASA imeunda kikosi kazi cha kushughulikia tatizo la upotevu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuimarisha miundombinu iliyopo hali itakayosaidia kuimarika kwa huduma ya maji katika maeneo yote yanayohudumiwa na Mamlaka hiyo.
Kwa sasa DAWASA imejikita katika kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwa wananchi zinaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza katika kutoa huduma bora kwa na kwa wakati ambapo Mamlaka hiyo imeweka mfumo unaowawezesha wananchi kuwasilisha taarifa pale ambapo kuna changamoto kupitia namba 0800110064.
Lengo la Mamlaka hiyo kukusanya Bilioni 12 kila mwezi linaonesha juhudi za makusudi zinazochukuliwa ambapo awali jukumu la kukusanya mapato lilikuwa chini ya DAWASCO ambayo sasa imeunganishwa na DAWASA na hivyo majukumu yote ya DAWASCO kuhamishiwa DAWASA, DAWASCO ilikuwa ikikusanya kati ya biloni 7 hadi 8 kwa mwezi.