Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

DAWASA Kutekeleza Miradi Saba ya Kimkakati 2023/24
Aug 11, 2023
DAWASA Kutekeleza Miradi Saba ya Kimkakati 2023/24
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Kiula Kingu akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 leo Agosti 11, 2023 kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) katika mwaka wa fedha 2023/24 imejipanga kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kupitia miradi saba ya kimkakati ikiwemo mradi wa Bwawa la Kidunda.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Bw. Kiula Kingu amesema hayo leo Agosti 11, 2023 katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu vipaumbele vya mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Bw. Kingu ametaja miradi mingine ya kimkakati inayotarajiwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha kuwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji, mradi wa maji Kwala, mradi wa maji Mji wa Pangani Kibaha, ujenzi wa mradi kutoka Kimbiji-Kigamboni hadi jirani na Chuo cha Uhasibu T.I.A, ujenzi wa mradi wa maji Kusini mwa Jiji la Dar es salaam na mradi wa uchimbaji visima virefu tisa eneo la Kigamboni.

“Miradi hii itakayotekelezwa kwa jumla ya shilingi bilioni 425.9 inalenga kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa yale ya pembezoni,” amesema Bw. Kingu.

Ameendelea kusema kuwa, DAWASA imejipanga kikamilifu kuchukua hatua za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira kupitia miradi mikubwa na midogo. Hii ni kwasababu upatikanaji wa maji unapoongezeka unapaswa uambatane na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira.

Aidha, kwa mwaka wa fedha uliopita 2022/23 DAWASA imetekeleza jumla ya miradi 10 ya kimkakati na zaidi ya miradi midogo midogo 86 ya kusogeza huduma kwa wananchi. Miradi hii ilihusisha kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa, kujenga matenki makuu yakuhifadhi maji, kujenga vituo vya kusukuma maji na kuongeza mtandao wa mabomba ya maji ili maji yanayozalishwa yanaweze kuwafikia wananchi ndani ya eneo la huduma.

“Miradi mikubwa iliyotekelezwa na kukamilishwa 2022/23 ni pamoja na, mradi wa ujenzi wa mfumo wa usambazaji maji kati ya Bagamoyo hadi matenki yaliyopo jirani na Chuo kikuu cha Ardhi, mradi wa maji Kigamboni, mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu, mradi wa maji Mshikamano, mradi wa maji nje ya mtandao (unaohudumia mitaa 12), mradi wa Maji Mbezi Makabe, mradi wa maji Zegereni, mradi wa maji Soga, mradi wa maji Mbwawa na miradi ya maji 14 iliyotekelezwa chini ya programu ya lipa kwa matokeo,” amesema Bw. Kingu.

Amesema miradi hiyo ina uwezo wa kuhudumia wakazi 722,308 katika mikoa ya Dar es salaam na Pwani ilijengwa kwa gharama ya jumla shiling bilioni 219.4

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi