Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, amesema utafiti uliofanywa na Wizara kwa kushirikiana na Wadau wa Shirika la 'Equality for Growth' mwaka 2019, kwa mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga umebaini kuwepo kwa unyanyasaji wa kijinsia kwenye masoko zaidi ya 20.
Akifungua Semina ya Siku moja kwa Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, Wenyeviti wa Masoko na Viongozi wa Shirikisho la Machinga nchini, SHIUMA wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani Oktoba 06, 2023 jijini Dar es Salaam, Mpanju amesema kufuatia utafiti huo Serikali kupitia Wizara iliamua kutengeneza Mwongozo wa Uanzishwaji na Uendeshaji wa Madawati ya Kijinsia kwenye Maeneo ya umma ili kukabiliana na changamoto ya vitendo vya ukatili.
“Pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuimarisha miundombinu ya masoko, bado kulionekana kuna changamoto ya vitendo vya ukatili kwenye maeneo hayo, kwani kuwa na masoko ni jambo moja lakini kama Serikali tuliona sio vema kuendelea kuacha vitendo hivyo viendelee kustawi badala yake tukaja na Mwongozo huu," amesema Mpanju.
Mpanju amesema, ingekuwa sio vema, baada ya utafiti wa 2019 katika masoko kuendelea kukaa kimya, kwani masoko ilikuwa ni kielelezo tu, bali vitendo hivyo vimetajwa kushamiri katika maenno ya vituo vya mabasi, mialo ya uvuvi, bichi na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu huku akitaja kundi la wanawake na watoto kuwa waathiriwa wakubwa.
Wakili Mpanju, amewataka viongozi hao, kutosubiri mafunzo ya mwongozo badala yake watendaji ngazi ya Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais –TAMISEMI kuusambaza mwongozo husika katika maeneo yote ya umma na kuanzisha madawati ya jinsia huku suala la mafunzo likitajwa kuwafikia kwa mujibu wa ratiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Rennie Gondwe, amebainisha kuwa Mikoa Sita imepatiwa mafunzo na zaidi ya mawadati 104 yameanzishwa, aidha baada ya mafunzo ya Dar es salaam jumla ya mikoa minane itakuwa imefikiwa na mafunzo kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara.
Naye Mwakilishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Esterina Sephania ameahidi kusimamia ipasavyo Uanzishwaji na Uendeshaji wa Madawati hayo ya Kijinsia katika mkoa huo kauli iliyoungwa mkono na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Shedrack Maxmilian.
Kwa mujibu wa Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi Esther Kaselenge, amesema, kwa awamu ya pili ya mafunzo wataifikia mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar Es Salaam, Mtwara, Lindi na Ruvuma ambapo jumla ya washiriki 300 wanatarajiwa kupatiwa mafunzo.