Na Tiganya Vincent, RS-Tabora
BODI ya Pamba Tanzania kwa kushirikiana Kampuni za usambazaji mbegu na dawa za kuua wadudu waharibifu zinatarajia kuanza kuepeleka jumla chupa 55,000 za viuawadudu katika Wilaya ya Igunga na Nzega mapema wiki ijayo.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkaguzi wa Pamba wa Wilaya ya Igunga George Kihimbi wakati akijibu swali la Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliyetaka kujua dawa hizo zitaanza kusambazwa kwa wakulima lini.
Alisema kuwa dawa hizo zinaweza kuhudumia hekari 55,000 za pamba katika maeneo yanayolima pamba Igunga na Nzega ili kuhakikisha mimea hiyo haishambuliwi na wadudu waharibifu.
Kihimbi alisema kuwa zoezi hilo litakwenda sanjari na usambazaji wa bomba za kupulizia dawa 1,000 kwa ajili ya kukabiliana na wadudu ambao wameanza kukata mimea ya wakulima.
Alisema kuwa kwa mabomba yaliyotumika msimu uliopita kama yatakuwa na matatizo yatakarabatiwa na Bodi ya Pamba ili yaweze kutumia tena.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri alisema kuwa kitendo cha uchelewaji wa dawa za kuua wadudu kuwafikia wakulima kinaweza kusababisha mavuno hafifu na hasara kwa wakulima na hivyo kuwavunja moyo baadhi yao.
Alisema kuwa njia pekee ya kuwasaidia wakulima ni pamoja na kuhakikisha dawa zinawafikia wakulima kwa wakati kama walivyofanya katika mbegu ili kuepuka mazao yao kuharibika na kupata hasara.
Mwanri alisema kuwa katika ziara yake ya ukaguzi wa mashamba ya wakulima ili kuojionea kama wamelima kwa kuzingatia Sheria na taratibu za ulimaji wa zao hilo kilio kikubwa cha wakulima ilikuwa ni kuwaishiwa dawa za kuua wadudu.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo aliwaagiza wakulima wa Pamba ambao mazao yao yameshaota vizuri kuanza kung’olea miche na kubakiza miwili ndani ya wiki nne.
Alisema kuwa kuchelewa kung’olea kunasababishia mimea ambayo haitakiwi kunyonya mbolea ya ile inayopaswa kubaki na hivyo kusababisha mavuno hafifu.