Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Chuo Kikuu cha California-Berkeley Waanzisha Ushirikiano na Chuo Kikuu Mzumbe
Oct 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Chuo Kikuu Cha California - Berkeley, Marekani, kimeanzisha mahusiano na ushirikiano na Chuo Kikuu Mzumbe ili kuimarisha na kukuza taaluma katika maeneo bobevu hususani maendeleo ya sayansi ya mazingira, utawala, sera na usimamizi.


Akizungumza wakati wa kikao na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, Prof. Youjin B. Chung, Mtaalamu wa Maendeleo ya Sayansi ya Mazingira, Sera na Usimamizi kutoka Chuo hicho amesema wamevutiwa na maeneo ya ubobevu na tafiti yanayotolewa na Chuo Kikuu Mzumbe na hivyo kuanzisha ushirikiano huo ni muhimu na bora baina ya vyuo hivyo kwani utasaidia kukuza maeneo ya utafiti na taaluma.


Akizungumza katika kikao hicho, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, amesema Mzumbe ni sehemu sahihi na bora ya kuanzisha, kukuza na kuendeleza ushirikiano katika maeneo ya ubobevu wa kitaaluma na tafiti na kwamba Chuo Kikuu Mzumbe kiko tayari kutoa ushirikiano katika kuhakikisha malengo ya ushirikiano baina ya vyuo hivyo yanafikiwa.


Akielezea hatua za ushirikiano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa na Baraza la Wahitimu, Dkt. Lucy massoi , amesema wamejizatiti kuhakikisha ushirikiano na taasisi za kimataifa zinazohusu tafiti na masuala ya elimu ya juu unaanzishwa na kuendelezwa, na kwamba tayari wameandaa mkataba wa mashirikiano na chuo cha Berkeley ambao unaonyesha maeneo ya ushirikiano, na utasainiwa wakati wowote ukisharidhiwa na pande zote.


Kikao cha Utambulisho na maridhiano kilifanyika Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro na kuhudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Chuo hicho.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi