Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Chuo cha Bandari Chajivunia Kutoa Wataalamu Bora Nchini
Nov 22, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Chuo cha Bandari kinajivunia kutoa wataalamu bora wengi ambao wamekuwa ni chachu ya mafanikio katika sekta ya uchukuzi na nyingine hapa nchini.

Hatua hiyo inatokana na takwimu kuonyesha kuwa fursa ya ajira kwa wahitimu wake ni zaidi ya asilimia 90 ambao huajiriwa katika maeneo mbalimbali ya sekta ya uchukuzi nchini.

Hayo yalibainishwa leo na Afisa Utawala Mwandamizi katika chuo hicho, Halima Kagobe wakati wakizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Tanga katika viwanja vya Bandari kunakoendelea mashindano ya SHIMMUTA.

Bi. Halima alisema kuwa kutokana na umahiri wa uwepo wa miundombinu bora ya kujifunzia umefanya chuo hicho kuweza kutoa wanafunzi ambao wanahitajika katika soko la ajira.

Aliongeza kuwa, kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia ambayo chuo hicho kinaenda sambamba kwa kuweka mitambo ya kisasa pamoja na kufundisha masomo ambayo yanaendana na hitajio la soko la ajira.

"Chuo chetu kina jukumu la kuandaa wataalamu ambao wataweza kutumika na TPA pamoja na sekta nzima ya uchukuzi", Alisema Kagobe.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo ya muda mfupi, John Leonard alisema kuwa kozi za uendeshaji wa mitambo kwa kipindi cha miaka ya hivi karibu imepata mwitikio mkubwa na vijana wa jinsia ya kike.

Alisema kuwa mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho sio tu yameweza kunufaisha wananchi wa hapa nchini pekee bali hadi nje ya nchi hususan zilizoko katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.

"Kwa sasa tumefanikiwa kufunga mashine ya kisasa ya kufundishia ambayo inajulikana kwa jina la "Simulation" ambapo imeongeza chachu ya washiriki kujifunza kozi za mashine katika chuo cha Bandari "Alisema

Alisema pia chuo hicho kinaendesha mafunzo ya utaalamu mbalimbali kama usimamizi wa forodha pamoja na usafirishaji kwa wadau mbalimbali katika sekta ya uchukuzi.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Chuo cha Bandari, Edda Mmari alisema wameshiriki kwenye mashindano ya SHIMMUTA yanayoendelea Jijini Tanga ili kutangaza chuo hicho ambapo alisema chuo kinatoa mafunzo katika eneo la Bandari hususan shughuli za utekelezaji, usalama na uendeshaji wa mashine za kupakia na kupakulia mizigo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi