Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuwekeza katika kutekeleza miradi ya Sekta ya Nishati nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Maendeleo ya Uchumi wa China, Liao Min wakati alipokutana na Waziri wa Nishati, January Makamba, Agosti 14, jijini Dar es Salaam na kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu ushirikiano katika uwekezaji na uendelezaji wa miradi ya Sekta ya Nishati inayofadhiliwa na China.
Katika mazungumzo yao, Min alimueleza Makamba kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya umeme kwa kuwa Tanzania imekuwa ikitoa matokeo chanya katika kila miradi inayofadhiliwa na nchi hiyo, hivyo kuifanya nchi hiyo kujenga uaminifu kwa Tanzania na kuendelea kushirikiana katika sekta ya nishati.
Waziri huyo wa China alieleza kufurahishwa kwake na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili na kueleza kuwa mwezi Novemba mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alitembelea nchi hiyo wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala, Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Decklan Mhaiki, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu na Mkurugenzi wa Utafutaji, Uendelezaji na Uzalishaji Mafuta na Gesi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), Kenneth Mutaonga.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, January Makamba ameishukuru Serikali ya China kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mikubwa katika sekta ya miundombinu ya usafiri na nishati kwa kujenga Reli ya TAZARA, madaraja makubwa, uwanja wa Mpira wa Benjamin Mkapa, uwanja wa Ndege wa Zanzibar na Ujenzi wa Bomba la kusafirisha Gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar Es Salaam.
Aidha, akizungumzia miradi ya Sekta ya Nishati, Makamba alisema nchi hiyo imewezesha utekelezaji wa miradi zaidi ya 11, ikiwemo ujenzi wa kuimarisha Gridi ya Taifa kwa Ukanda wa Kaskazini na Mashariki, Ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania ( EACOP), Kituo cha kupoza na kupokea umeme cha Chalinze na maeneo mbalimbali nchini.
Makamba alitaja fursa zingine zilizopo katika sekta ya nishati ambayo nchi ya China inaweza kuendelea kushirikiana na Tanzania.
Fursa hizo ni pamoja na kuimarisha Gridi ya Taifa, Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta na Gesi katika kina kirefu cha bahari, na Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini.
Vilevile alieleza kuwa nchi hizo zibadilishane wataalam ili kujifunza zaidi, kuongeza ujuzi na ufanishi katika sekta husika, pia wafanye utafiti ili kuibua miradi mipya itakayoweza kutekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizo.
Pamoja na mambo mengine aliweka wazi matokeo chanya yaliyopatikana wakati wa ziara yake nchini China mwezi Juni mwaka huu kuwa ni kuwepo kwa kampuni zaidi tisa ya pamoja na taasisi mbili zinazotaka kuja kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati katika kuendeleza miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati.