Na Lilian Lundo - Chato
Wakazi wa Wilaya ya Chato wamempongeza Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa ya kukamilisha miradi yote iliyoachwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli.
Pongezi hizo, zimetolewa katika ziara ya Rais Samia ya kufungua hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato iliyoko wilayani humo, leo.
"Chato tunamshukuru Rais Samia, na tunaona anavyojali ahadi zake alizosema kwamba atatekeleza mipango yote aliyoacha Hayati Magufuli, na sasa tumeona hospitali kubwa ya rufaa iliyokamilika ujenzi wake hapa Chato," amesema Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Chato, Samweli Bigambo.
Ameendelea kusema kuwa, wakazi wa wilaya hiyo ilikuwa ikiwalazimu kusafiri mpaka Mwanza kwenda hospitali ya Bugando au Dar es Salaam hospitali ya Muhimbili kwa ajili kupata matibabu ya Kibingwa.
Lakini kwa sasa huduma hizo wanazipata wilayani kwao kupitia hospitali hiyo kanda.
"Hata mimi nimeanza kutibiwa hospitalini hapo, magonjwa ambayo yangeweza kunisafirisha kwenda nje ya Chato, lakini sasa hivi tunatibiwa hapa hapa Chato," amesema Mzee Bigambo.
Ameendelea kusema kuwa, wilaya hiyo kwa sasa inashuhudia idadi kubwa za shule ambazo zimejengwa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambako kwa sasa kila kijiji ina shule ya Sekondari ili kila mtoto wa Kitanzania aweze kupata elimu iliyo bora.
Kwa upande wake, Rehama Samweli, ambaye ni fundi nguo wilayani Chato amesema anamshukuru Rais Samia kwa kuwapelekea hospitali ya kanda wilayani humo.
"Tulikuwa tunahangaika kwenda kutibiwa mbali, lakini kwa sasa hivi hospitali ya kanda ipo hapa karibu, itatupa wepesi hata wenye kipato kidogo tutakuwa tunatibiwa hapa karibu," amesema Rehema.
Ameendelea kusema kuwa, hospitali hiyo itasaidia ukanda wote wa Ziwa Victoria pamoja na nchi jirani kama vile Uganda, ambapo tayari wameanza kuja hospitalini hapo kupata matibabu mbalimbali ya kibingwa.