Jonas Kamaleki.
Chama cha Labour cha nchini Uingereza kimepongeza juhudi za Rais John Pombe Magufuli na Serikali yake kwa utendaji mzuri katika kulinda na kugawanya rasilimali kwa watu wake.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Viongozi wa Labour Party katika Mkutano na vyama mbali mbali vya kisiasa vikiwemo vya Kiafrika vya SWAPO, ANC na CCM, uliofanyika Uingereza kama anavyoeleza Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa kimataifa, Kanali (Mstaafu) Ngemela Lubinga katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii.
“Chama cha Labour kinataka haki sawa kwa wote, kwa hiyo kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kusimamia rasilimali na kuhakikisha rasilimali zetu zinazoibiwa zisiibiwe tena, kimewapa faraja,” alisema Lubinga.
Lubinga amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inasimamia rasilimali kitendp ambacho kitaleta maandeleo kwani hakuna maendelo yanyowezakupatikana bila usimamizi wa rasilimali.
“Chama cha Labour kinapigana kuhakikisha wananchi wake wanapata makazi bora, hivyo suala la Accacia ambao walikuwa wakifanya vitendo visivyoendana na hali halisi ya rasilimali hasa kwetu sisi walengwa kimewafurahisha sana na kuona kuwa mazungumzo yamekamilika katika mazingira ya kukubaliana namna ya rasilimali hizo zinavyotumika kuwanufaisha watanzania,”alisema Lubinga.
Kuhusu mwelekeo wa uchumi, Kanali (Mstaafu) Lubinga amesema kuwa uchumi wa Tanzania unakua na utakuwa wa kuvutia kwani juhudi za makusudi zinafanyika hivyo amewataka wanachi wawe na subira.
Ameongeza kuwa wazazi wawaandae watoto wao kufanyakazi na wasiwaachie tu kwenda wanavyotaka. Ametoa mfano kuwa mtu akiona mtoto wake amenunua gari la kifahari inabidi amuulize fedha ametoa wapi za kununua gari hilo wakati mshahara wake unajulikana na ni mdogo.
Amewataka watanzania wawe wavumilivu kwani mabadiliko huleta kiwewe kwa wat na yakishaleta matokeo chanya, watu hao husahau walioleta maendeleo hayo.
Serikali ya Awamu ya Tano imetimiza miaka miwili tangu iingie madarakani tarehe 5 Novemba, 2015. Katika kipindi hiki watanzania wameshuhudia miradi mikubwa ya maendeleo ikianzishwa na kutekelezwa, mfano ujenzi wa barabara,madaraja, ununuzi wa ndege sita, ujenzi wa reli ya kisasa, (standard gauge), utengenezaji wa madawati na elimu bure kwa elimu ya msingi na mwisho nidhamu ya kazi imerejea katika utumishi wa umma.