Frank Mvungi- Maelezo, Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswaada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania ya Mwaka 2017 (The Tanzania Telecomunications Corporation Bill, 2017) mapema leo mjini Dodoma ikiwa ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kuimrisha sekta ya Mawasiliano.
Akizungumza wakati akijibu hoja za Wabunge waliochangia muswada huo Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa kuanzishwa kwa Shirika hilo kutawanufaisha wananchi walio wengi hasa wanaoishi maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu hali itakayochochea kukua kwa uchumi nchini.
“Kuanzishwa kwa Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania kutawanufaisha Watanzania wote kutokana na fursa zitakazojitokeza katika maeneo yote ya nchi yetu zikiwemo ajira kwa kuwa Shirika hili halitabagua Watanzania katika swala la ajira ilimradi mhusika ana sifa stahiki ” Alisisitiza Prof. Mbarawa
Akifafanua amesema kuwa kuwepo kwa Shirika hilo kutasaidia kuimarisha ushindani katika sekta ya Mawasiliano hapa nchini kwa kuwa Muundo wa shirika hilo utabadilika na hata utendaji wake utajikita katika kuongeza tija na kulinda maslahi ya Taifa.
Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona kuwa shirika hilo linafanya kazi kwa tija na kuzalisha faida hali itakayopelekea Serikali kupata gawio kutokana na faida iliyozalishwa.
Aidha Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali imepokea maoni ya wabunge kuhusu kuongeza mtaji wa Shirika hilo ili liweze kuongeza tija katika kutoa huduma kwa wananchi.
Bunge limepitisha Muswaada wa Sheria ya Kuanzishiwa kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2017 ambapo Shirika hilo pamoja na mambo mengine litakuwa na jukumu la kuimarisha mawasiliano nchini, kulinda Usalama, kukuza uchumi na masuala ya Kijamii.