Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

BUCKREEF Yakonga Moyo wa Waziri Biteko kwa Kutoa Ajira kwa Wazawa
Jul 17, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameupongeza mgodi wa dhahabu wa Buckreef kwa kutoa ajira kwa Watanzania wanaofanya kazi mbalimbali za uzalishaji wa dhahabu katika mgodi huo.


Dkt. Biteko amebainisha hayo Julai 16, 2022 wakati alipotembelea mgodi wa Buckreef mkoani Geita ili kujionea maendeleo ya shughuli za ujenzi na uchimbaji madini katika mgodi huo. 


Amesema, mgodi wa Buckreef umetoa ajira za moja kwa moja 354 kwa Watanzania katika nafasi mbalimbali katika mgodi huo.


Amesisitiza kwa wafanyakazi waliopewa ajira katika mgodi huo kuhakikisha wanajenga taswira nzuri kwa kuwa wazalendo na waaminifu katika kazi zao. 


Amesema, kupitia uaminifu wawekezaji watatoa fursa zaidi kwa Watanzania kuweza kufanya kazi mbalimbali.


Aidha, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, miradi yote iliyopo kwenye Sekta ya Madini itaendelezwa ili watanzania wanufaike na rasilimali madini na kuongeza Pato la Taifa. 


"Matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kwamba miradi yote ambayo ipo kwenye Sekta ya Madini iweze kuendelezwa,"amesisitiza.


Kwa upande wake, Mkuu Mkoa wa Geita, Rosemary ameupongeza mgodi wa Buckreef kwa kusimamia usalama kwa wafanyakazi. 


Aidha, amemuomba Dkt. Biteko kuhakakisha Serikali inaleta Wawekezaji wengi mkoani Geita kutokana na mkoa huo kuwa na maeneo mengi ya uwekezaji katika Sekta ya Madini.


Naye, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buckreef, Gaston Mujwahuzi amesema wataendelea kuwashirikisha wananchi katika huduma za kijamii kwa ajili ya manufaa ya watu wote. 


Aidha, shughuli nyingi za manunuzi ya vifaa mbalimbali yanafanyika hapa nchini ili kuhakikisha manufaa ya uwekezaji yanabaki kuwa ya Watanzania.


Kampuni ya Dhahabu ya Buckreef ikishirikiana na Mbia mwenza Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) inajushughulisha na uchimbaji wa madini ya dhahabu. Pia Kampuni ya Buckreef inamiliki hisa kwa asilimia 55 na STAMICO inamiliki hisa asilimia 45.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi