Kampuni ya ndege ya British Airways imetangaza kurejesha safari za moja kwa moja kati ya Uingereza na Tanzania kuanzia Mei 2027, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za utalii, biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.
Tangazo hilo limetolewa Oktoba 7, 2026 na Mkuu wa Masoko wa British Airways kwa Bara la Afrika, Asia na Pasifiki, Bw. Moran Birger, katika Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza lililofanyika jijini London akieleza kuwa uamuzi huo umechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya watalii na wasafiri wanaoitembelea Tanzania, pamoja na maendeleo ya kiuchumi na ongezeko la uwekezaji nchini.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amepongeza uamuzi huo na kueleza kuwa kurejea kwa British Airways kutaendelea kuifungua Tanzania kwa dunia na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi na Taifa.
Amesema Tanzania ina nafasi ya kuwa kitovu cha uwekezaji kwa masoko ya kikanda, hivyo wawekezaji wanapaswa kulitazama Taifa hilo kama jukwaa la kuwafikia wadau wa nchi mbalimbali.

Dkt. Mwigulu amesema amani, utulivu na uongozi imara, pamoja na miundombinu ya barabara, SGR, bandari, viwanja vya ndege na upatikanaji wa umeme wa uhakika, ni miongoni mwa mambo yanayowezesha ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini.
Amesema mageuzi ya kiuchumi yanayotekelezwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 yanahitaji pia umeme wa uhakika na wa gharama nafuu ili kuongeza uzalishaji na ushindani wa uchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali imeandaa sera, mipango na malengo thabiti kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa, kwa lengo la kufungua fursa za uwekezaji na kuwezesha ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.