Na: Frank Mvungi
Serikali imeridhishwa na kasi ya uzalishaji viatu katika Kiwanda cha BORA ambacho ni moja ya viwanda vilivyobinafsishwa na kushindwa kuendelezwa kwa kipindi kirefu hadi pale Serikali ilipotangaza kuvitwaa tena viwanda ambavyo havijaendelezwa.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika kiwanda hicho leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage amesema ziara hiyo ililenga kukagua na kuona jinsi maagizo ya Serikali kwa wamiliki wa viwanda vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji yanavyotekelezwa ikiwemo kuongeza uzalishaji na kuweka mitambo ya kisasa.
“BORA ni moja ya Kiwanda kilichokuwa hakifanyi vizuri lakini leo nimejionea mwenyewe kuwa sasa wameanza kuwa Kiwanda cha mfano kwa kuzalisha viatu vyenye ubora kwa kiwango cha Kimataifa nah ii inaonyesha kuwa Tanzania ya Viwanda inawezekana” Alisisitiza Mhe. Mwijage
Akifafanua Mhe Mwijage amesema kuwa kiwanda hicho kinapaswa kuongeza mitambo zaidi ili kuongeza zaidi uzalishaji unaoendana na mahitaji ya soko kwa kuwa kwa sasa Taasisi za Serikali na zile za Binafsi zina mahitaji makubwa ya bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho kikongwe hapa nchini.
Akizitaja bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda hicho Mhe. Mwijage kuwa ni pamoja na viatu vya usalama, raba, viatu vinavyotumika Hospitalini na vile vya michezo na soli za viatu.
Pia Mhe. Mwijage alitoa rai kwa wale wote waliobinafsishiwa viwanda kuviendeleza vinginevyo watanyanganywa mara moja kwa kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanda vyote vilivyopo nchini vinazalisha bidhaa kulingana na mahitaji ya soko hali inayoongeza ajira.
Kwa upande wake Meneja Biashara na Uhusiano wa Kiwanda hicho Bw.Sylivery Buyaga amesema kuwa kiwanda hicho kimewekeza zaidi ya bilioni 7 kwa kununua mitambo mipya na ya kisasa ambayo imesadia kuboresha uzalishaji hali iliyochochea wateja kuongezeka.
“Mafundi wetu tunachukua kutoka VETA na hawa wanakuwa wamefuzu mafunzo yao kwa kiwango kinachokubalika hali ambayo imetusaidia kuzalisha bidhaa zenye ubora na kwa mwaka tunazalisha zaidi pea laki 600,000 za viatu vya shule kwa ajili ya wanafunzi ikiwa ni sehemu ya bidhaa tunazozalisha.” Alissisitiza Buyaga.
Ziara ya Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage katika kiwanda cha kuzalisha Viatu cha BORA ni sehemu ya ufuatiliaji wa agizo la Serikali lililowataka wale wote wanaomiliki viwanda walivyobinafsishiwa kuviendeleza ili kuendana na dhana ya Serikali kujenga uchumi wa Viwanda.