Na Veronica Simba - REA
Bodi ya Nishati Vijijini inayosimamia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imehitimisha muda wake kisheria na kupongezwa kwa kutekeleza majukumu yake kwa juhudi, weledi, uadilifu na uzalendo.
Akizungumza mwishoni mwa juma, katika hafla fupi ya kuwaaga Wajumbe wa Bodi hiyo, mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali aliwaeleza kuwa Serikali inatambua mchango wao katika majukumu mbalimbali waliyotekeleza, hususani katika kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini hadi kufikia asilimia 69.8.
Mahimbali ambaye alimwakilisha Waziri wa Nishati, alieleza majukumu mengine yaliyotekelezwa na Bodi hiyo kwa ufanisi mkubwa ni pamoja na kuongezeka uunganishaji umeme kwa wateja wa vijijini kutoka 584,639 hadi kufikia wateja 956,511 sawa na asilimia 63.6.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kusimamia kuongezeka kwa Mfuko wa Nishati Vijijini kutoka Shilingi Bilioni 1,337 hadi Bilioni 1,684 sawa na asilimia 26. Aidha, kuongezeka kwa michango ya wabia wa maendeleo kutoka Shilingi Bilioni 252 hadi Bilioni 560 sawa na asilimia 123 pamoja na kusimamia kikamilifu maslahi ya wafanyakazi wa Wakala.
Naibu Katibu Mkuu alieleza zaidi kuwa, Bodi ilisimamia kikamilifu utekelezaji wa jukumu la msingi la Wakala ambalo ni kuhamasisha na kuwezesha upatikanaji wa nishati bora vijijini ili kuboresha maisha ya wananchi waishio vijijini, kiuchumi na kijamii kupitia upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo kuifanya Serikali kutembea kifua mbele kwa mafanikio yaliyopatikana ambayo yameacha alama Tanzania na Afrika nzima.
“Kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru kwa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Nishati Vijijini kwa uadilifu mkubwa na maslahi mapana ya Taifa. Kwa hakika, kazi hii ni ngumu na inahitaji watu wenye uadilifu na uzalendo wa hali ya juu kutekeleza majukumu haya kama mlivyofanya ninyi.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Julius Kalolo, alitoa shukrani kwa Serikali, Wabia wa Maendeleo, Wizara ya Nishati, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa REA, kwa ushirikiano wa hali na mali katika kuiwezesha Bodi kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Wakili Kalolo alifafanua kuwa, kitendo cha Serikali na Wabia wa Maendeleo kuendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya nishati vijijini kimeiwezesha Bodi hiyo kupata mafanikio yote iliyofikia.
Aidha, alisema kuwa ushirikiano uliotolewa na wafanyakazi wote wa REA, Wizara na Taasisi mbalimbali zinazohusiana na Wakala huo, umechangia kwa kiasi kikubwa kufikia mafanikio hayo.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya Wajumbe wenzake wa Bodi, Mkurugenzi Dailin Mghweno alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaamini na kuendelea kuwapa nafasi ya kuwatumikia Watanzania hadi walipohitimisha muda wao.
Naye Mkurugenzi, Mhandisi Francis Songela aliahidi kuwa Wajumbe wote wa Bodi hiyo wataendelea kutoa ushirikiano kwa REA na Serikali kwa ujumla katika kuhakikisha malengo yote yaliyopangwa kutekelezwa yanafikiwa.
“Tutaendelea kuwa Mabalozi wazuri na tuko tayari muda wote kutoa ushirikiano pale utakapohitajika,” alisisitiza Mhandisi Songela.
Katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi aliwatunuku tuzo na vyeti maalum kama ishara ya kutambua utumishi wao uliotukuka ambao umeleta tija katika sekta ya nishati vijijini.
Wajumbe wa Bodi hiyo iliyoteuliwa Januari 31, 2019 na ambayo imehitimisha muda wake wa miaka mitatu kisheria ni Mhandisi Styden Rwebangila akiwakilisha Wizara ya Nishati, Dailin Mgweno (Umoja wa Walaji Tanzania), Mhandisi Francis Songela (Wabia wa Maendeleo), Louis Accaro (Sekta Binafsi), Frolian Haule (Vyama vya Ushirika) na CPA Oswald Urassa (Umoja wa Benki Tanzania).