Na Mwandishi wetu- MAELEZO
Katika kuelekea miaka 61 ya Uhuru, Bodi ya Nyama Tanzania itahakikisha inasimamia vizuri Tasnia ya Nyama ili nyama inayozalishwa iwe bora na salama kwa mlaji.
Hayo yameelezwa na Msajili wa Bodi hiyo, Dkt. Daniel Mushi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo pamoja na vipaumbele vyake
“Bodi itaendelea kuhamasisha uzalishaji bora wa nyama hapa nchini ili nchi ifaidike na ongezeko la masoko ya nyama nje ya nchi yaliyotokana na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia diplomasia ya uchumi”. Amesema Dkt. Mushi.
Aidha, amebainisha kuwa Bodi hiyo itashirikiana na mamlaka nyingine kuhakikisha vituo atamizi vya vijana wanaofanya unenepeshaji wa mifugo vinafanikiwa na vinakuwa endelevu, kama njia ya kuongeza wigo wa ajira kwa vijana, na pia kuvihakikishia viwanda vya nyama malighafi bora pamoja na kulinda masoko yaliyopo.
Fauka ya hayo Dkt. Mushi ameeleza kuwa, Bodi hiyo ina mkakati wa kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo kwenye mnyororo wa uzalishaji nyama na bidhaa za nyama zikiwemo machinjio, viwanda vya kuchakata nyama, mifumo ya ubaridi na unenepeshaji.
“Kuongezeka kwa ubora na usalama wa nyama inayopatikana sokoni na kulinda afya za wananchi kupitia mafunzo yanayotolewa na Bodi ya Nyama na ukaguzi wa kazi za wadau utasaidia wazalishaji wa nyama na bidhaa zake kufikia viwango vya kitaifa na kimataifa”. Amebainisha Dkt Mushi.