Wananchi jijini Dodoma wamempongeza Mhe. Dkt. Dotto Biteko kwa kuapishwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Bunge kumpongeza rasmi leo.
Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dodoma, kufuatia uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan unaozingatia utendaji kazi wa mtu, uzalendo na nidhamu yake.
“Kwa uchapaji wake wa kazi na unyenyekevu wake, na uteuzi huu alioupata ni dhahiri kwamba Rais Samia anazingatia utendaji kazi wa mtu katika teuzi anazozifanywa, tunampongeza kwa uteuzi na kuapishwa kuwa Naibu Waziri Mkuu,” ameeleza Joseph Solomon alipohojiwa na mwandishi wa habari hii kwenye Soko la Sabasaba.
Naye, Bi. Warda Karimu amesema, “alipokuwa Waziri wa Madini, aliisimamia vyema sekta hiyo iliyokuwa inayumba kwa miaka mingi, alihakikisha analinda rasilimali za nchi bila uwoga, alimsaidia vyema Rais.”
Mhe. Dkt. Dotto Biteko ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe tangu mwaka 2015. Katika nafasi yake ya Naibu Waziri Mkuu, Watanzania wote wakiwa na Imani kwamba atasimamia vyema utekelezaji wa shughuli za serikali.