Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni Mbili Kukamilisha Ujenzi Chuo cha VETA Sumbawanga
Feb 07, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na OMM - Rukwa

Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Rukwa kwa kutoa shilingi Bilioni 2.035 kazi ambayo imeanza tayari.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mwishoni mwa wiki hii, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti alisema Rais Samia Suluhu Hassan tayari ameshatoa fedha hizo ambapo kazi imeanza kupitia Mshauri Mkandarasi Chuo cha Ufundi Arusha.

“Tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi 2,035,364,881 zitakazokamilisha mradi huu wa chuo cha VETA Sumbawanga ambao ulikwama miaka miwili iliyopita. Sasa ndani ya miezi mitatu ijayo mradi unakwenda kukamilika”, alisema Mkirikiti.

Mkirikiti alimtaka msimamizi wa mradi huo Chuo cha Ufundi Arusha kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati na kuwa anatakiwa kutoa taarifa ya ujenzi na changamoto atakazopitia kila mwezi ili kutokwamisha jitihada za Serikali.

“Hapa tumelaza uchumi mkubwa baada ya mradi kusimamia miaka miwili iliyopita, sasa hatutakubali mradi huu ukwame tena wakati fedha tunazo. Lengo kazi hii ikamilike kwa ubora na kwa wakati ili watu wapate faida ya mradi huu katika kubadilisha hali za kiuchumi za wana Rukwa”, alisisitiza Mkirikiti.

Mkuu huyo wa Mkoa aliyetembelea eneo hilo la mradi akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa, alitaja faida za uwepo wa chuo hicho cha VETA kuwa kitazalisha ujuzi kwa vijana wa Rukwa katika fani za ufundi sanifu, kuchochea ukuaji, ajira kwa vijana na akina mama pamoja na ujasiriamali.

Naye Msimamizi wa Kazi za Ujenzi toka Chuo cha Ufundi Arusha, Dennis Emanuel alisema wamesaini mkataba wa kazi kuanzia Februari Mosi mwaka huu na kuwa wanatarajia kukabidhi mradi ifikapo mwezi Mei mwaka 2022.

Dennis aliongeza kuwa wamejipanga kukamilisha kazi zote kwa kutumia mafundi bora ambapo tayari kazi za kusafisha mazingira na kukusanya vifaa vya ujenzi imeanza.

Mradi wa ujenzi chuo cha VETA Sumbawanga hadi uliposimama ujenzi ulikuwa umejenga mabweni ya wanafunzi, madarasa, vituo vya mafunzo kwa vitendo, mkataba, jengo la utawala na mifumo ya maji na umeme ambavyo vitakamilishwa awamu hii kufuatia serikali kutoa fedha hizo.

Kazi mpya zitakazofanyika sasa ni pamoja na ujenzi wa mabweni mapya mawili pamoja na nyumba ya Mkuu wa Chuo.

Kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Rukwa ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Mpango wa Ustawi na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TRCP No. 5441).

Mkazi wa Sumbawanga Monica Sokoni anayefanya kazi ya kibarua kwenye mradi huo alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za kufanikisha mradi huo kwani umemuwezesha tena kupata ajira.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi