Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

BIlioni 8 Kuboresha Miundombinu ya Elimu 2023/2024
Aug 10, 2023
Mamlaka ya Elimu Tanzania
Na Lilian Lundo – MAELEZO

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imepanga kutumia shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini katika mwaka huu wa fedha 2023/24.

Mkurugenzu Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bi.  Bahati Geuzye amesema hayo leo Agosti 10, 2023 katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma, alipokuwa akieleza vipaumbele vya mamlaka hiyo katika mwaka wa fedha 2023/24.

Bi. Bahati amesema kuwa, kiasi hicho cha fedha kitatumika kufadhili miradi 82 katika shule 81 zikiwemo shule 48 za msingi na 33 za sekondari katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara. Amesema kuwa miradi hiyo itakapokamilika itanufaisha wanafunzi39,484 na walimu 169 katika shule za msingi na sekondari.

“Miradi itakayofadhiliwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 82, matundu ya vyoo 336, mabweni 10, ujenzi wa maabara 18 za masomo ya sayansi na nyumba za walimu 32,” amesema Bi. Geuzye.

Pia katika mwaka huu wa fedha TEA itatoa ufadhili kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunza na kufundisha katika taasisi moja ya elimu ya juu Zanzibar. Mradi huo umepangwa kutumia shilingi milioni 300 katika utekelezaji wake.

Aidha katika mwaka wa fedha uliopita 2022/23 kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na TEA iligharamia ufadhili wa shilingi bil. 10.99 kwa miradi 132 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151.

“Miradi hiyo ilijumuisha ujenzi wa madarasa 114 katika shule 38 (msingi 36 na sekondari 02), maabara 10 za sayansi katilka shule 5 za sekondari, matundu ya vyoo 888 katika shule 37 (msingi 29 na sekondari 08), miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na utoaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule 08 za msingi,” amesema Bi. Geuzye.

Mfuko wa Elimu unapata fedha kutokana na vyanzo vya kisheria vilivyoanishwa katika Sheria ya Mfuko wa Elimu no. 8 ya mwaka 2001 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2013. Vyanzo hivyo ni pamoja na tengeo la kibajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Pia unapokea michango ya fedha na vifaa kutoka kwa wadau wa elimu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi