Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Jumla ya Shilingi 4,413,700,000 zimetengwa katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima TEWW.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Taasisi ya TEWW, Dkt. Michael Ngumbi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji na vipaumbele kwa mwaka huu wa fedha.
“Zaidi ya Shilingi bilioni 4.4 ya matumizi ya maendeleo zitatumika katika kutekeleza programu ya SEQUIP kwa Shilingi 1,000,000,000, programu ya IPOSA Shilingi 946,000,000, uendelezaji miundombinu ya majengo na TEHAMA, ununuzi wa vifaa na vitendea kazi pamoja na uboreshaji wa maktaba kwa Shilingi 1,967,700,000 na ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la utawala katika kampasi ya Morogoro kwa Shilingi 500,000,000,” amesema Dkt. Ngumbi
Dkt. Ngumbi ameongeza kuwa kwa mwaka 2022/2023, TEWW inatarajia kuendelea na utekelezaji wa jukumu la kukamilisha mtaala wa mafunzo ya walimu wa elimu ya watu wazima katika maeneo ya ufundi na teknolojia na kupata idhini ya NACTVET.
Aidha, ameyataja maeneo ya kipaumbele ya taasisi hiyo kuwa ni kuimarisha usajili na usimamizi wa watoa huduma za elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi katika ngazi ya elimu ya msingi na kuimarisha uendeshaji na utoaji mafunzo kwa walimu na wasimamizi wa elimu ya watu wazima nchini.
Pia, kuimarisha uandaaji mitaala, mihtasari na machapisho yanayohusu elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi na kuimarisha uratibu na uendeshaji kampeni mbalimbali za kitaifa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wadau mbalimbali katika masuala mtambuka.
Dkt. Ngumbi ametoa wito kwa wananchi kujiunga na programu za elimu ya watu wazima zinazotolewa na TEWW kwa sababu ni taasisi inayotoa elimu kwa nadharia na vitendo kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuwa mtu bora, mwenye uwezo wa kujiendeleza na kupambana na changamoto za maisha.