Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 3 Kupeleka Umeme Visiwani, Mbali na Gridi ya Taifa
Aug 18, 2023
Bilioni 3 Kupeleka Umeme Visiwani, Mbali na Gridi ya Taifa
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 18, 2023 kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wakala hiyo na mwelekeo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 katika Ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma
Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema mradi wa kupeleka Umeme katika visiwa na maeneo yaliyombali na Gridi ya Taifa ni mradi unaojumuisha ujenzi wa mifumo midogo ya kusambaza umeme  katika maeneo yenye vyanzo vya nishati jadidifu kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji.

Mhandisi Saidy amebainisha hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 18, 2023 katika Ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wakala hiyo na mwelekeo kwa mwaka wa Fedha 2023/24.


Akifafanua  zaidi, Mhandisi Saidy anasema  "Mikataba miwili ya miradi wa Ikondo - Matembwe Hydro Power ulisainiwa mwezi Februari 2023 na mkataba wa mradi wa Mwenga Hydro Power ulisainiwa mwezi Machi  2023, miradi hiyo itaunganisha jumla ya wateja wa awali 2,168 katika vijiji 42 kwa gharama ya Shilingi 3.06 bilioni".

Aidha, Serikali kupitia REA imewapata waendelezaji watatu wa miradi ya kusambaza umeme kwa kutumia nguvu ya jua, itakayotekelezwa katika visiwa 28 vilivyopo katika mikoa ya Kagera (8), Mwanza (13), Mara (3) na Lindi (4) na hivyo kuunganisha wateja 9,515 kwa gharama ya Shilingi bilioni 11.18.

Kwa upande wa  mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya Wachimbaji Wadogo wa Madini, Viwanda na Kilimo, Mhandisi Said ameeleza kuwa mradi huo unahusu  kupeleka umeme katika maeneo 114 ya wachimbaji wadogo wa madini, maeneo 222 ya kilimo na viwanda katika mikoa 25 Tanzania Bara.

"Mradi unatarajiwa kuunganisha wateja wa awali 19,187 kwa gharama ya shilingi bilioni 115 ikiwa ni fedha za ndani. Aidha, mradi wa kupeleka umeme katika Shule na Mahakama za Mwanzo Vijijini, Mradi huu unahusu kupeleka umeme katika shule 729 na mahakama za mwanzo 292 vijijini ambazo hazina umeme", amefafanua Mhandisi Saidy.

REA na TANESCO wapo katika hatua za mwisho za kusaini makubaliano ambapo TANESCO itafanya kazi ya kuzipelekea umeme katika Shule na Mahakama hizo na REA itakua inatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi