Na Ahmed Sagaff
Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekadiria kutumia shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kuendeleza Ubunifu na Utengenezaji wa Vifaa vya TEHAMA katika Mwaka wa Fedha 2022/23.
Hayo yameelezwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Fedha hizo zitatumika kujenga Kituo cha Kuendeleza Wataalam, tafiti na ubunifu wa TEHAMA na kufanya maandalizi ya ujenzi wa makao makuu ya Tume ya TEHAMA, kuwezesha shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya mradi na kuanzisha vituo vya ubunifu na Atamizi TEHAMA katika wilaya mbili.
Kazi nyingine ni kutengeneza mfumo jumuishi utakaounganisha usajili na uendelezaji wa wataalam na wabunifu TEHAMA nchini na kukiendeleza kituo cha kuendeleza kampuni changa za TEHAMA cha Dar es Salaam na kujenga vituo viwili vya Kanda vya kutengeneza bidhaa za TEHAMA.