Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bilioni 18.4 Zanunua Vifaa Tiba Chato
Oct 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Lilian Lundo - MAELEZO 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 18.4 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato. 


Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato, Brian Mawalla amesema hayo katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii. 


"Rais ametupa vifaa tiba vya shilingi bilioni 18.4 na fedha za ujenzi takribani shilingi bilioni 33.6, kwa fedha hizi alizozitoa hatutakiwi kumuangusha Rais wetu, tutaendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania na wagonjwa wa nchi jirani," amefafanua Dkt. Mawalla. 


Ametaja vifaa tiba vilivyosimikwa katika hospitali hiyo kuwa ni pamoja na mashine 10 za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, mashine mbalimbali za mionzi ikiwemo CT-Scan, Echo ya kisasa na MRI. 


Amesema hospitali hiyo inatoa huduma za kibingwa na kibingwa bobezi katika upande wa moyo, figo, maabara, mionzi, upasuaji, na upande wa akina mama na watoto, ambapo imeanza kutoa huduma hizo tangu tarehe 31/07/2021 na mpaka sasa wameona jumla ya wagonjwa 15,000 wakiweno wagonjwa kutoka nchi jirani ya Burundi.

Aidha, amesema kuwa, uwepo wa hospitali hiyo wilayani  Chato imewapunguzia wagonjwa adha ya kusafiri kwa umbali  mrefu kutafuta matibabu, pamoja na kuwapunguzia gharama ya kwenda kutafuta matibabu. 


Naye, Adeline Teobabu, Mkazi wa Chato ambaye amempeleka mtoto wake hospitalini hapo kupata matibabu, amemshukuru Rais Samia kwa kuwawezesha kupata hospitali ya kisasa katika wilaya yao. 


"Hospitali ni nzuri na ya kisasa, pia tunapata huduma nzuri kutoka kwa madaktari na manesi wa hospitali hii, nilimleta mwanangu alikuwa anaumwa, lakini kwa sasa a anaendelea vizuri. Tunamshukuru sana Rais Samia kwa hospitali hii, kwani huduma zote za kimatababu tunazipata karibu na nyumbani," amesema Adeline.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi