Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bil. 93.8 Zatumika Kuboresha Miundombinu ya Shule 588
May 22, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo - Dodoma

Katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2018/19, zaidi ya shilingi Bilioni 93.8 zimetumika katika uboreshaji wa miundombinu ya shule 588 ambapo shule  303 ni za msingi na sekondari 285.

Hayo yameelezwa leo, Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bumbwini, Muhammed Amour Muhammed juu ya juhudi zipi za makusudi ambazo Serikali inakusudia kuchukua ili kupandisha hali ya ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha Nne.

 "Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ufaulu katika ngazi mbalimbali za Elimu. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu katika shule mbalimbali za Serikali nchini," amesema Ole Nasha.

Ole Nasha amesema kuwa uboreshaji wa miundombinu uliofanyika katika shule hizo 588 umehusisha madarasa 1,190, mabweni 222, vyoo 2,141, mabwalo 76 na nyumba 99.

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo, vifaa vya maabara katika shule, na vifaa vya kielimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Aidha Naibu Waziri Ole Nasha ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Aprili 2019 Serikali imeajiri jumla ya walimu 17,884 ili kukabiliana na uhaba wa walimu nchini.

Vile vile Serikali imeendelea kuimarisha Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule kwa kununua na kusambaza magari 45 ya Uthibiti Ubora wa Shule na Pikipiki 2,897 kwa ajili ya Maafisa Elimu kata na kuongeza kuwa katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 Serikali inatarajia kujenga ofisi 100 za wathibiti ubora wa shule na kuongeza idadi ya watumishi.

Aidha amesema ufaulu wa wanafunzi katika mtihani wa kidato cha IV umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka 2018 watahiniwa waliofaulu ni asilimia 78.36 ikilinganishwa na asilimia 77.09 ya mwaka 2017, asilimia 70.35 ya mwaka 2016 na asilimia 67.91 ya mwaka 2015.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi