Na Ahmed Sagaff, MAELEZO
Juhudi za Serikali za kuboresha mazingira wezeshi ya biashara ya kemikali nchini zimeifanya biashara hiyo kuongezeka katika Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema Serikali imeweza kufanya mapitio ya Sheria ya Kemikali na kuruhusu biashara kubwa ya kemikali aina ya Sulphur inayoingizwa nchini kwa wingi katika mfumo wa kichele.
“Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, vibali vya uingizaji wa kemikali viliongezeka kufikia 63,588 ikilinganishwa na vibali 49,234 vilivyotolewa Mwaka wa Fedha 2020/2021 ikiwa ni ongezeko la vibali 14,354.
“Mbali na utoaji vibali vya kemikali, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022 imefanikiwa kusajili wadau wanaojihusisha na shughuli za kemikali 1,087 ikilinganisha na wadau 1057 waliosajiliwa kwa Mwaka Fedha 2020/2021 ikiwa ni ongezeko la wadau 30”, ameeleza Dkt. Mafumiko.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni tasisi ya Serikali iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sheria Na. 8 ya Mwaka 2016.