Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Biashara kati ya Tanzania na India imekua na kufikia dola za kimarekani bilioni 3.1 kwa mwaka 2022.
Akizungumza katika ziara ya Kikazi aliyoifanya nchini India Oktoba 9, 2023 Rais Samia amesema kuwa Tanzania na India zina ushirikiano wa kihistoria wa miaka mingi na kwamba ushirikiano huo umefanya biashara kati ya nchi hizo mbili kukua.
"Napenda kutoa shukrani kwa Serikali na Watu wa India kwa ushirikiano wenu wa miaka mingi katika sekta mbalimbali, kwenye sekta ya biashara kati ya Tanzania na India imekua na kufikia dola za kimarekani bilioni 3.1 mwaka 2022 na kufanya India kuwa namba 3 kwenye eneo hilo lakini pia kuwa namba 5 kati ya nchi zilizowekeza nchini kwetu,” amesema Mhe. Rais Samia.
Ameendelea kusema kuwa Tanzania itaendelea kufungua fursa zaidi za ushirikiano na India kwenye maendeleo ya kiuchumi na kisiasa huku akiipongeza India kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa G-20.
Aidha, Rais Samia alimshukuru Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi kwa ukarimu na ukaribisho mzuri waliouonesha kwake pamoja na ugeni wake nchini humo
Aliongeza kuwa Tanzania na India zinaendelea kufurahia ushirikiano wa miaka mingi ambao ni wa kihistoria na ziara hiyo inathibitisha utayari wa Tanzania kuendelea kuimarisha urafiki huo.