Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Benki ya Kilimo Tanzania Kufungua Ofisi za Kikanda Kwa Awamu
Apr 20, 2018
Na Msemaji Mkuu

Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

Serikali imeeleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) inatekeleza Mpango wa Miaka Mitano (2017- 2021), wa kusogeza huduma karibu na wateja kwa kuanzisha ofisi za Kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kusini, Kati, Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar kwa awamu.

Hayo yameelezwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu maswali ya msingi ya Mbunge wa Viti Maalumu Mhe.  Jacqueline Msongozi (CCM), aliyetaka kujua lini Serikali itapeleka Benki ya Kilimo katika Mkoa wa Ruvuma ili wananchi waweze kukopeshwa.

Aidha, Mhe. Msongozi alitaka kufahamu utayari wa Serikali kupunguza riba ya mikopo wanayokopeshwa Wakulima katika Benki hiyo.

Akijibu maswali hayo, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa  hadi kufikia Juni 30, 2018  Ofisi ya Kanda ya Kati, Dodoma, itakuwa imefunguliwa ambayo pia itakuwa ni Makao Mkauu ya Benki hiyo.

 “Baada ya ufunguzi wa ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika Benki Itafanya uchambuzi wa fursa zilizopo Kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu za kufungua ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha”, alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa Benki hiyo inatoa mikopo kwa kutumia mfumo wa makundi, kundi la kwanza wakulima wadogo wadogo kwa riba ya asilimia 8- 12, kundi la pili la miradi mikubwa ya kilimo kwa asilimia 12 – 16 kwa mwaka na kundi la mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko la matumizi ya mkopo.

Kuhusu kupunguza riba kwa wakopaji, Dkt. Kijaji alibainisha kuwa majadiliano ya kiwango cha riba yanaweza kufanyika kulingana na historia ya mkopaji.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi