Jumla ya madawati 120 yenye thamani ya shilingi 24,000,000 yatakayokaliwa na wanafunzi 360 yametolewa na Benki ya KCB Tanzania kwa Halmashauri ya Mji Kibaha ili kutatua changamoto ya wanafunzi wa Shule za Msingi kukaa chini
Makabidhiano hayo yamefanyika tarehe Oktoba 12, 2023 kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo ambapo mgeni maalum alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Mhe. Silvestry Koka.
Afisa Elimu Msingi na Awali, Bernadina Kahabuka ameeleza kuwa Kibaha Mji ina wanafunzi 42,487 wa Shule za Msingi za Serikali ikiwa na mahitaji ya madawati 14,162 hata hivyo yaliyopo ni 10,623 hivyo kupungukiwa 3,539
Kahabuka kando ya kuishukuru Benki ya KCB Tanzania amempongeza Mbunge kwa jitihada anazozifanya kwa kuwatafuta wadau na kupata madawati 120 yanayokwenda kuboresha ufaulu kwa watoto 360
Akiongea kwa niaba ya uongozi wa Benki ya KCB-Tanzania, Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Christine Manyenye amesema tangu waanze kutoa huduma za Kibenki mwaka 1997 wamekuwa wakisaidia kwenye sekta za Elimu,Afya hasa kwa wakinamama wajawazito, watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na maafa ya Kitaifa na bajeti imekuwa ikiongezwa kila mwaka ili kuleta utawi wa jamii.
Aidha, amesema Benki yao inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Elimu, hivyo wameamua kumuunga mkono kwa vitendo ili kukidhi ndoto zake za kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora, hata hivyo ametoa rai kwa Walimu kuhakikisha madawati hayo yanatunzwa ili yaweze kutumika kwa kipindi kirefu
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Mhe.Silivestry Koka amemshukuru na Kumpongeza Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya wafanyabiashara ikiwemo Benki ya KCB Tanzania ambao hivi sasa wanatambua mchango wake na kuamua kuunga mkono maendeleo ya nchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mhandisi Mshamu Munde ameeleza changamoto za sekta hiyo kuwa ni miundombinu ya majengo na samani ikiwemo madarasa, nyumba za Walimu, maktaba, mabweni kwa shule za Sekondari, vyoo na samani kama viti na meza kuwa ndivyo vinavyosaidia katika kufikisha elimu bora na kwamba mchango uliotolewa na Benki ya KCB Tanzania ni njia ya kuelekea kwenye mafanikio.
"Pamoja na kuwa Serikali yetu chini ya Rais wetu, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan imeelekeza nguvu kubwa kwenye Sekta ya Elimu, elimu bure imekuwa ni chachu ya uandikishaji watoto wengi kila mwaka, hivyo hii ni changamoto ya kimaendeleo kwa Taifa", amesema Koka.