Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuitengea Tanzania jumla ya Dola za Marekani bilioni 2.1 sawa na Shilingi trilioni 4.9 katika mzunguko wa 20 wa IDA (Julai 2022 – Juni 2025) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi pamoja na kupunguza umasikini wa watu wake.
Dkt. Nchemba ametoa shukrani hizo wakati akizungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayoendelea Mjini Washington DC, Marekani.
Kati ya kiasi hicho, jumla ya Dola za Marekani milioni 535 sawa na asilimia ishirini na tano ya mgao tayari zimeshaidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Kusambaza Umeme Vijijini (Dola za Marekani milioni 335) na Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (Dola za Marekani milioni 200).
Aidha, Bodi hiyo inatarajiwa kuidhinisha Dola milioni 150 hivi karibuni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi maji safi na usafi wa mazingira vijijini.
Pamoja na jitihada hizo za Benki, Mheshimiwa Mwigulu alimuomba Bi. Kwakwa, kuisaidia Tanzania fedha za ziada takribani Dola za Marekani bilioni 1.7 ili kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kipaumbele kupitia fedha za mzunguko wa IDA-20.
“Bado tuna mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi yetu ya kimkakati itakayochochea kwa kasi ukuaji wa uchumi wetu, hivyo naiomba Benki ya Dunia ikubali kutuongezea Dola za Marekani bilioni 1.7 katika mzunguko wa IDA 20 ili tuweze kukamilisha miradi 18 ya kimkakati tuliyoiwasilisha Benki ya Dunia ukiwemo mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa-SGR”, alisema Dkt. Nchemba.
Akizungumza katika Mkutano huo, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayezisimamia nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, aliipongeza Tanzania kwa hatua mbalimbali inazozichukua katika kusimamia uchumi na maendeleo ya wananchi wake. Aliahidi kuwa Benki yake iko tayari kuendelea kuisadia Tanzania ili iweze kufikia malengo yake ya maendeleo kwa kuipatia fedha na utaalam utakaosaidia nchi kufikia malengo yake.
Bi. Kwakwa aliahidi kuwa Benki yake itasaidia pia jitihada za Serikali za kukuza kilimo ili Tanzania iwe ghala la chakula kwa nchi zote za Ukanda wa Kusini na Mashariki na duniani kwa ujumla na pia kusaidia miradi ya kijamii kama maji na hifadhi ya mazingira.
Kuhusu maombi yaliyowasilishwa na Tanzania kusaidia ujenzi wa Reli ya Kisasa-SGR, Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia aliahidi kuyafanyia kazi na kwamba atawaelekeza watalaamu kupitia nyaraka muhimu za mradi huo ili kuangalia maeneo ambayo Benki hiyo itaweza saidia utekelezaji wa mradi wa SGR.
Aidha, Bi. Kwakwa alipongeza jitihada za Serikali za kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara hatua itakayovutia mitaji na uwekezaji kupitia mpango wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Mpaka sasa Benki ya Dunia imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 7.2, sawa na takriban Shilingi za Tanzania trilioni 16.7 kwa ajili ya kutekeleza miradi zaidi ya 29 nchini Tanzania ambapo kati ya miradi hiyo, 24 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.41 ni ya kitaifa na mingine 5 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 0.75 ni ya kikanda.