Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, amewaagiza Mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mikoa yote kufanya upembuzi yakinifu na kubaini maeneo yote korofi ya barabara na kuyawasilisha Wizarani ili yaweze kupewa kipaumbele wakati wa kuandaa bajeti.
Bashungwa, ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, Mhe. Katani Ahmed aliyetaka kujua ni lini Serikali itatenga fedha ya dharura kujenga kipande cha Barabara ya Nguja - Mkwiti - Tandahimba yenye maeneo Korofi.
“Nitumie nafasi hii kuwaelekeza Mameneja wa TANROADS mikoa yote kuangalia maeneo yote korofi na kufanya upembuzi yakinifu na kuyawasilisha Wizarani ili yapewe kipaumbele wakati wa kuandaa bajeti”, amesema Bashungwa
Aidha, Mbunge wa Tandahimba, Mhe. Katani Ahmed alitaka kujua Je, ni lini ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara kutoka Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala hadi Masasi utaanza, ambayo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020 na ni ahadi ya Mhe. Rais.
Wakati akijibu swali hilo, Bashungwa amesema ujenzi wa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi yenye urefu wa kilometa 210 unatekelezwa kwa awamu ambapo ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mtwara – Mnivata (km 50) umekamilika kwa kutumia fedha za ndani.
Bashungwa amesema kuwa sehemu ya barabara ya Mnivata – Newala - Masasi (km 160) chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesainiwa tarehe 21 Juni, 2023 kwa sehemu za Mnivata – Mitesa (km 100) na Mitesa – Masasi (km 60) pamoja na ujenzi wa Daraja la Mwiti, kwa sasa Makandarasi wa sehemu zote mbili wapo katika hatua za maandalizi ya kuanza ujenzi.