Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Barabara ya Sale – Ngarasero Kujengwa kwa Kiwango cha Lami
Dec 20, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa Serikali imedhamiria kujenga barabara inayoanzia Sale hadi Ngarasero (km 50) kwa kiwango cha lami ili kufungua uchumi wa Ngorongoro, kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji na kukuza utalii.

Aidha, ameiagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kuanza usanifu wa sehemu ya barabara ya Wasso – Loliondo (km 10) ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Prof. Mbarawa amesema hayo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, wakati akikagua mradi wa barabara ya Mto wa Mbu – Loliondo (km 217) sehemu ya Wasso – Sale (km 49), inayojengwa kwa kiwango cha lami na kumtaka mkandarasi China Wu Yi kukamilisha barabara hiyo mapema mwanzoni mwa mwaka 2022.

“Serikali kwa kujua umuhimu wa eneo hili imeamua kujenga barabara hii kwa awamu, tunamaliza kilometa 49 sasa na kuanza na kilometa 50 nyingine ili wananchi waweze kusafiri kwa kutumia barabara ya lami”, amefafanua Waziri Mbarawa.

Aidha, amewataka wananchi wa maeneo hayo kuitunza na kuilinda barabara hiyo kwa kutopitisha hovyo mifugo katika barabara pamoja na kuharibu alama za barabara ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

“Ninawaomba wananchi wa hapa ambao ni wafugaji wazuri muilinde hii barabara na mifugo ipite katika maeneo maalum yatayotengwa kupitisha mifugo”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi Mshauri wa mradi kutoka TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU), Mhandisi Mbaraka Shafi, ameeleza kuwa mradi umefikia asilimia 97 na unaratajiwa kukamilika ifikapo mwezi Aprili, 2022.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, amemueleza Waziri huyo changamoto wanazozipata katika utekelezaji wa miradi ikiwemo wanapotangaza zabuni mara nyingi watu hawafiki eneo hilo kutokana na jiografia ngumu ya wilaya hiyo.

“Kupata mkandarasi huku ni ngumu hivyo kwa kuwa mkandarasi huyu tayari ana vifaa vyote na anaujua uzoefu wa huku angepewa barabara zingine ili tuweze kuufungua kwa haraka mkoa wa Arusha na Mara”, amesema Mangwala.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ameipongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mkoa wa Arusha kwa usimamizi na ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na kuwataka wakamilishe jengo hilo mapema iwezekanavyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi