Immaculate Makilika – Chunya, Mbeya
Wakazi wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wameishukuru Serikali kwa kujenga barabara ya Chunya – Makongolosi yenye urefu wa kilomita 39 ambayo imegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 6 inatajwa kurahisisha shughuli za usafirishaji na biashara kwa wakazi hao.
Akizungumza leo wilayani Chunya mkoani Mbeya katika mahojiano maalum na Idara ya Habari – MAELEZO, Bw. Samson Mtenga mkazi wa Makongolosi amesema kuwa barabara hiyo imekuwa msaada kwao kwani sasa shughuli zao za biashara na usafirishaji zimekuwa rahisi.
“Kwetu sisi hii barabara ni neema kubwa hapo awali tulikua tunatumia saa hata sita kwenda Mbeya kwa vile barabara ilikuwa mbaya lakini sasa hivi tunatumia saa chache zaidi kwenda Mbeya” alisema Mtenga.
Vilevile Bw. Mtenga amewaomba wananchi wa Makongolosi kutunza miundombinu hiyo ya barabara kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya maendeleo.
Naye, Khamis Daudi mkazi wa Makongolosi amesema kuwa barabara hiyo imewasaidia kusafiri kwa wakati na hivyo kuwapa nafasi ya kutosha kufanya shughuli zingine za kiuchumi.
“Kabla ya hii barabara kutengenezwa kutoka hapa Makongolosi hadi Mbeya nauli ilikuwa Shilingi 12,000/= baada ya barabara nauli ilifika Shilingi 5,000/= hata hivyo kwa sababu ya gharama za mafuta nauli ni Shilingi 7000/= kwa kweli tunaishukuru Serikali kwa kuwa tunategemea bidhaa kutoka mjini kuja hapa” amesema Daudi
Aidha, Beatrice Bilali, mkazi wa Wilaya ya Chunya amesema kuwa barabara hiyo imekuwa mkombozi kwa wanawake kwa vile awali akina mama wajawazito wamewahi kupoteza watoto wakati wa kusafirishwa kuelekea hospitalini.
“Tunamshukuru Mhe. Rais kwa hii barabara kabla ya sasa akina mama tulikuwa tunateseka kwa uchungu wa uzazi na uchungu wa barabara kwa jinsi ilivyokuwa mbovu na makorongo mengi na hivyo watoto wetu wengine walifika barabarani lakini sasa hilo hali haipo tena tunaishukuru sana Serikali kwa kusikia kilio chetu” Amesisitiza Beatrice.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania, Mhandisi Rogatus Mativila ametaja baadhi ya viwango wa ujenzi wa barabara hiyo kuwa ni upana wa mita 9.5, madaraja makubwa matatu, makaravati madogo 23, mifereji iliyojengwa kwa zege, alama za usalama barabarani, taa za barabarani 57 katika zilizowekwa katika Kijiji cha Mtumbasi na taa za barabarani 39 zilizowekwa katika mji wa Mkongolosi.
Barabara hiyo ya Chunya - Makongolosi ambayo imezinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani humo ni sehemu ya barabara ya Mbeya – Chunya – Makongolosi – Singida ambayo ikikamilika itaunganisha mikoa mitatu ya Mbeya, Tabora na Singida ambapo pia itaunganisha nchi za kusini na mashariki mwa Tanzania.