Na Beatrice Lyimo - CHINA
Balozi wa Tanzania nchini China Mhe. Mbelwa Kairuki amezitaka Taasisi zenye dhamana ya kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali nchini ikiwemo TANTRADE , Bodi ya Kahawa, Bodi za Chai, Korosho, Nafaka na Mazao mchanganyiko kushiriki kwenye maonesho mbalimbali yatakayofanyika nchini China ili kutafuta masoko mapya ya bidhaa zao.
Balozi Kairuki ameyazungumza hayo alipokutana na ujumbe wa Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi walipotembelea nchini China kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu baina ya China na Tanzania katika tasnia ya habari na mawasiliano.
"Uzoefu wa hivi karibuni umekuwa wa kukatisha tamaa kutokana na Ubalozi kutafuta fursa mbalimbali kwa ajili ya bidhaa za Tanzania kutangazwa lakini wadau wameshindwa kushiriki" ameongeza Balozi Kairuki.
Aidha, Balozi Kairuki amesema kuwa kumekuwepo na ongezeko la matumizi ya kahawa miongoni mwa Watu wa Jamhuri ya China na kahawa ya Tanzania ni miongoni mwa kahawa zinazopendwa sana na watu hao hivyo hiyo ni nafasi ya kupata soko la uhakika nchini humo endapo itafanyika kampeni mahususi ya kuitangaza kahawa ya Tanzania.
Vilevile amesema kuwa Madini mbalimbali na vito kutoka Tanzania yana nafasi ya kupata soko nchini China endapo patakuwepo na mifumo mizuri ya kisasa ya kuendesha mnada ya madini.
Mbali na hayo, Balozi Kairuki ametaja baadhi ya matarajio ya Ubalozi wa Tanzania nchini China katika kipindi cha miaka minne ijayo ikiwepo kuongeza idadi ya sasa ya watalii toka China kutoka 30,000 hadi 100,000 ifikapo mwaka 2020.
Aidha, amesema kuwa Ubalozi unatarajia kuongeza uwekezaji kutoka China hususani kwenye ujenzi wa viwanda ikiwa na lengo la kati ya sasa hadi 2021 kuvutia viwanda 100 ili kufanya ongezeko la uwekezaji kutoka dola za Kimarekani Bilioni 3.6 za sasa hadi kufika dola za Kimarekani bilioni 7 ifikapo 2021.
"Pia Ubalozi unatarajia kuongeza idadi ya fursa za mafunzo kwa Watanzania katika fani mbalimbali hususani uhandisi ikiwa na lengo kuu la kuhakikisha watanzania 1,000 wapate mafunzo ya uhandisi ifikapo mwaka 2021.
Dkt. Abbasi ameambatana na baadhi ya Wakuu wa Vitengo vya Habari na Uhusiano Serikalini wa Wizara na Taasisi za Serikali kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu baina ya Tanzania na China katika sekta ya mawasiliano.